Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS imesimamisha uanachama wa Guinea katika mkutano wa kilele wa viongozi wa jumuiya hiyo baada ya wanajeshi wa nchi hiyo kuiangusha serikali ya rais Alpha Conde.
Katika taarifa kwa waandishi wa habari, waziri wa mambo ya nje wa Burkina Faso Alpha Barry,aliyeshiriki kwenye mkutano huo wa viongozi wa nchi 15 za ECOWAS uliofanyika jana jioni kwa njia ya video, mjini Ouagadougou amesema Guinea kwa sasa imesimamishwa kwenye mabaraza yote ya kupitisha maamuzi ya jumuiya hiyo ya ECOWAS.
Waziri wa mambo ya nje wa Burkina Faso amefahamisha kwamba jumuiya hiyo sasa itauomba Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuidhinisha uamuzi wake huo. Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Burkina Faso amesema ujumbe wa upatanishi wa jumuiya hiyo utakwenda hii leo Alhamisi katika mji mkuu wa Guinea, Conakry kufanya mazungumzo na mamlaka mpya.