Jumuiya kuu ya kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, imekataa pendekezo la utawala wa kijeshi wa Niger la kufanya uchaguzi ndani ya miaka mitatu, na kuzidisha mzozo wa kisiasa ambao unaweza kusababisha uingiliaji wa kijeshi, iwapo hakuna makubaliano yataafikiwa kufuatia mapinduzi ya mwezi Julai.
ECOWAS na wasuluhishi wengine wenye nguvu, wamekuwa yakitafuta suluhu za kidiplomasia, kwa mapinduzi hayo ya Julai 26 nchini Niger, ambayo ni ya saba katika ukanda wa Afrika Magharibi na Kati, katika kipindi cha miaka mitatu.
Lakini baada ya juhudi kadhaa kushindikana, jumuiya hiyo - ambayo imechukua msimamo mkali zaidi kuhusu Niger kuliko majirani zake wanaoongozwa kijeshi - ilianzisha kikosi cha kikanda ambacho wakuu wa kijeshi wamesema kiko tayari kupelekwa nchini humo iwapo mazungumzo hayatafanikiwa.
Ijumaa wiki jana, ECOWAS ilisisitiza, kwa mara nyingine, tishio lake la kuingilia kijeshi, siku moja kabla ya serikali ya kijeshi hatimaye kukubali kukutana na ujumbe wa ECOWAS katika mji mkuu Niamey, na kupelezea nia mpya ya kushirikiana.
Katika hotuba yake kwa taifa kwenye televisheni Jumamosi jioni, kiongozi wa serikali ya kijeshi Jenerali Abdourahamane Tiani, alisema viongozi wa mapinduzi bado wako tayari kwa mazungumzo.
Kamishna wa ECOWAS Abdel-Fatau Musah aliambia Reuters siku ya Jumatatu kwamba msimamo wa jumuiya hiyo bado uko wazi, kwamba ni lazima utawala wa kikatinba urejeshwe mara moja, na kiongozi aliyeondolewa, Mohamed Bazoum, aachiliwe huru.