Juhudi hizo zinafanyika wakati ECOWAS ikiiendeleza msimamo wake wa kutishia kuingilia kati kijeshi kwenye taifa hilo katika mzozo huo mkubwa uliozivuta nchi zenye nguvu duniani.
Jumuiya hiyo, jana Jumamosi ilisema kwamba imedhamiria kutuma kamati ya bunge ili ikutane na viongozi wa mapinduzi ambao wanamshikilia Rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum, na wameshavunja serikali yake. Mapinduzi ya kijeshi ya Niger ni ya saba Afrika ya Magharibi na Afrika ya Kati katika kipindi cha miaka mitatu.
Msemaji wa bunge la ECOWAS amesema kuwa licha ya kuwa bunge hilo halikufanya maamuzi thabiti Jumamosi, liliunda kamati inayopanga kuonana na Rais wa Nigeria Bola Tinubu ambaye kwa sasa anakalia uenyekiti wa kupokezana ili ipate ruhusa yake ya kwenda Niger.
Viongozi wa mapinduzi wakiongozwa na Jenerali Tiani, wamekataa juhudi za awali za kidiplomasia za ECOWAS, Marekani na nchi nyingine jambo linaloweza kuongeza mzozo katika kanda masikini ya Sahel ambayo tayari inakabiliwa na makundi ya itikadi kali.
Kutokana na mzozo huo, si tu hatma ya Niger ambayo ni mzalishaji mkubwa wa madini ya Urani na mshirika wa mataifa ya magharibi katika vita dhidi ya makundi ya itikadi kali iliyo mashakani, bali pia ushawishi wa mataifa hasimu yenye nguvu duniani ambayo yana maslahi ya kimkakati kwenye eneo la Afrika Magharibi na Afrika ya Kati.
Wanajeshi wa Marekani, Ufaransa na Italia wako Niger, katika ukanda ambao washirika wa ndani wa al Qaeda na kundi linalojiita dola la Kiislamu wameshawauwa maelfu ya watu na kuwafanya mamilioni wayakimbie makazi yao.