Jumuia ya uchumi ya nchi za Afrika magharibi Jumatano imesema uingiliaji wa kijeshi katika nchi ya Niger inayotawaliwa na wanajeshi “itakuwa hatua ya mwisho”, huku Nigeria ikisitisha usambazaji wa umeme kwa Niger ili kuzidisha shinikizo kwa viongozi wa mapinduzi nchini humo.
Na huku Ufaransa, mtawala wa zamani wa kikoloni wa Niger ilipeleka ndege ya tano kuondoa raia wake, kiongozi wa mapinduzi Jenerali Abdourahamane Tiani alisisitiza kuwa hakuna sababu yoyote kwa raia wa Ufaransa kuondoka nchini Niger.
Wakuu wa majeshi ya nchi wanachama wa ECOWAS walikutana jana katika mji mkuu wa Nigeria Abuja ili kutafuta suluhu wakati wajumbe wa jumuia hiyo walikuwa nchini Niger kwa mazungumzo, wiki moja baada ya mapinduzi yaliyotikisa taifa hilo dhaifu.
Viongozi wa ECOWAS siku ya Jumapili walichukua viikwazo vya kibiashara na kifedha, na kuwapa viongozi wa mapinduzi wiki moja ili kumrejesha madarakani rais wa Niger aliyechaguliwa kidemokrasia au wakabiliwe na uwezekano wa matumizi ya nguvu.
“Suluhisho la kijeshi ni njia ya mwisho kabisa mezani, suluhisho la mwisho, lakini lazima tujiandae ikibidi kufanya hivo,” alisema Abdel-Fatau Musah, kamishna wa ECOWAS wa masuala ya kisiasa, amani na usalama.
Ujumbe wa ECOWAS unaoongozwa na rais wa zamani wa Nigeria Abdulsalami Abubakar ulikuwa Niger kwa mazungumzo, aliongeza wakati wa uzinduzi wa mkutano wa siku tatu wa wakuu wa majeshi mjini Abuja.