Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EAC yatenga bajeti dola milioni 97, vipaumbele 7

D2b7127a7915f67c5ee18613ddf24f1f EAC yatenga bajeti dola milioni 97, vipaumbele 7

Tue, 18 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BARAZA la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki limepitisha makadirio ya bajeti ya jumuiya hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ya dola za Marekani milioni 97.6.

Baraza hilo katika mkutano wake wa kawaida wa 41 uliofanyika hivi karibuni kwa njia ya mtandao, lilipitisha bajeti hiyo itakayotumika kuhudumia taasisi tatu za jumuiya na shughuli za maendeleo kwa mwaka huu wa fedha ulioanza Julai Mosi, 2020 hadi Juni 30, 2021 na kutangaza vipaumbele saba.

Kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 55.6 zitapatikana kutokana na michango ya nchi sita wanachama, huku wadau wa maendeleo wakichangia dola milioni 41.9.

Vyombo vikuu vya EAC ni sekretarieti ya jumuiya, Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) na Mahakama ya Afrika Mashariki, pamoja na taasisi za Tume ya Bonde la Ziwa Victoria na Shirika la Uvuvi la Ziwa Victoria.

Nyingine ni Baraza la Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, Tume ya Utafiti wa Afya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Mashariki, na Mamlaka ya Ushindani ya Afrika Mashariki.

Katika kikao hicho, Baraza la Mawaziri lilipitisha bajeti ya matumizi ya kawaida inayokadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 2.7 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya Shirika la Afrika Mashariki linaloshughulikia masuala ya anga (Cassoa) .

Nchi wanachama pia zitachangia kupitia mamlaka zao za anga katika mwaka huo wa fedha inayokadiriwa kila nchi kutoa dola za Marekani 458,910.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki, Dk Vincent Biruta, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Rwanda, alisema bajeti hiyo itapelekwa katika Bunge la Jumuiya hiyo kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa mwezi huu.

Katika bajeti hiyo, EAC imeweka vipaumbele vikubwa saba, ikiwamo Umoja wa Forodha katika bidhaa zinazoingizwa katika jumuiya na za ndani ya jumuiya ikiwamo za kilimo na bidhaa nyingine zinazotumika kwa wingi.

Pia, maendeleo ya Miundombinu katika ukanda huo yamepewa kipaumbele, kuwezesha uingizaji wa bidhaa zote za viwanda katika jumuiya na maeneo mengine ya ushirikiano chini ya soko la pamoja na sarafu ya pamoja.

Kipaumbele kingine ni kuboresha sekta ya viwanda kupitia uwekezaji, maendeleo ya ujuzi na uboreshaji wa teknolojia na ubunifu ili kukuza maendeleo ya uchumi.

Vingine ni uboreshaji wa uzalishaji wa bidhaa za kilimo, kuongeza thamani na kuwezesha usambazaji wa bidhaa za kilimo kuwezesha usalama wa chakula, kuhamasisha amani, ulinzi na utawala bora katika ukanda huo na mabadiliko katika taasisi za ukanda huo na nchi wanachama.

Baraza hilo pia limehuwisha mikataba ya wafanyakazi wataalamu 25 katika vyombo vya EAC na taasisi zake walioajiriwa mwaka 2015 na mikataba yao inamalizika au inatarajiwa kumalizika mwisho wa Agosti, mwaka huu katika awamu ya mwisho ya miaka mitano kulingana na masharti ya sheria na kanuni za wafanyakazi wa EAC (2006).

Baraza lilipitisha utoaji wa mikataba mipya kwa wafanyakazi ya muda mfupi kwa muda wa miezi sita kutoka Julai Mosi hadi Desemba 31, mwaka huu.

Mbali na Dk Biruta, mkutano huo wa siku moja, pia ulihudhuriwa na mawaziri wa nchi wanachama wanaoshughulikia masuala ya EAC ambao ni Adan Mohammed (Kenya), Balozi Ezechiel Nibigira (Burundi), Deng Alor Kuol (Sudan Kusini), Meja Jenerali Kahinda Otafiire (Uganda) na Dk Damas Ndumbaru (Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania).

Chanzo: habarileo.co.tz