Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EAC yajivunia ushiriki wanawake katika utawala

7897e2bdf1e8f27a89e54ad223a832a2.jpeg EAC yajivunia ushiriki wanawake katika utawala

Tue, 16 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SEKRETARIETI ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imejivunia maendeleo yaliyopatikana katika kukuza ushiriki wa wanawake katika utawala, ingawa kumekuwapo na mapungufu kadhaa.

Hayo yamebainika katika hotuba ya Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko iliyosomwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Sekretarieti ya EAC, Ruth Simba, akisema kuwa licha ya maendeleo yaliyopatikana ndani ya jumuiya katika kukuza ushiriki wa wanawake katika utawala, mapungufu yanabaki katika uwakilishi wa wanawake katika ngazi tofauti za uongozi .

“Hali hiyo ipo katika ngazi za chini na baadhi ya Mashirika na Taasisi za jumuiya hivyo ni lazima kufanyiwa kazi,” alisema Balozi Mfumukeko.

Alisema hayo wakati EAC wakifanya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika wiki iliyopita yakiwa na kaulimbiu “Wanawake katika Uongozi: Kufikia Mustakabali sawa katika dunia ya Covid-19.”

Katika maadhimisho hayo, Jaji Mkuu anayemaliza muda wake katika Mahakama ya Haki Afrika Mashariki, Jaji Monica Mugenyi alipewa tuzo ya mwaka ya mwanamke bora katika uongozi kwenye ukanda huu.

“Hata tunaposherehekea mafanikio mengi ambayo sisi kama EAC tumepata katika uwezeshaji wa wanawake na wasichana, hatupaswi kusahau kamwe kwamba wanawake bado wanapambana kuinua hadhi yao kwani katika jamii nyingi wanachukuliwa kama raia wa daraja la pili. Wananyimwa fursa za kutimiza matakwa yao ya kiuchumi na kisiasa,” aliongeza Balozi Mfumukeko.

Alipongeza kazi kubwa iliyofanywa na wanawake Afrika Mashariki na kwingineko wakati wa janga la Covid-19.

“Wakati shule zimefunguliwa tena katika nchi washirika, tuligundua kuwa idadi kubwa ya wanafunzi hasa watoto wa kike wameshindwa kuendelea na shule kwa sababu ya mimba za utotoni,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Christophe Bazivamo alisema bado kuna changamoto nyingi EAC ambazo zinapaswa kushughulikiwa kama vile unyanyasaji wa kijinsia (GBV), unyanyasaji wa mwilini, ubakaji, ukeketaji kwa watoto wa kike (FGM) na ndoa za mapema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz