Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EAC yaipongeza Tanzania miradi ya kimkakati

F0f8a849461ad5239dcc045ff6f23afa EAC yaipongeza Tanzania miradi ya kimkakati

Tue, 22 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imeeleza kufurahishwa na miradi mikubwa na ya kimkakati, inayotekelezwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jumuiya hiyo imesema kukamilika kwa miradi hiyo, kutachochea ukuaji wa uchumi na biashara katika jumuiya nzima na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji. Pongezi hizo zilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayeshughulikia Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala, Steven Mlote.

Alisema hayo akiwa na ujumbe wa jumuiya hiyo wakati walipotembelea mradi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani. Mradi huo mkubwa unatarajiwa kukamilika Juni 2022 na utazalisha megawati 2,115 za umeme. Mlote alieleza kuvutiwa na taarifa ya mradi huo kufadhiliwa na fedha za Watanzania wenyewe.

Alimpongeza Rais John Magufuli kwa maono hayo. Pia alipongeza mradi huo kutoa zaidi ya ajira 5,000 ambapo asilimia 90 ni Watanzania. Awali, kabla ya kutembelea mradi huo, ujumbe huo wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ulitembelea Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wake.

Ulieleza kufurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Tanzania. Mlote aliwasihi vijana wa Tanzania waliopata fursa za ajira katika ujenzi wa reli hiyo, kujifunza kwa moyo na kujituma ili kupata maarifa na ujuzi wa kuendelea kutunza na kuendesha hata baada ya wataalamu kutoka nje wanaohusika na ujenzi huo kuondoka nchini.

Alitoa wito kwa Watanzania, hasa ambao wanazunguka eneo la miradi hiyo, kuitunza na kuilinda kwa kuwa manufaa yake ni makubwa ikiwamo kuongeza uzalishaji wa mazao na bidhaa za viwandani na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Chanzo: habarileo.co.tz