Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EAC yaidokeza Guinea mambo yaliyofanikisha ' mtangamano'

Dfc99d69e4c82ab8c4da372c13d61580 EAC yaidokeza Guinea mambo yaliyofanikisha ' mtangamano'

Tue, 31 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imetaja mambo yaliyofanikisha ajenda yake ya mtangamano ikisema ni pamoja na dhamira ya juu ya kisiasa.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa EAC, Dk Peter Mathuki, Mkurugenzi wa Sekta za Jamii katika Sekretarieti ya (EAC), Stephen Niyonzima, alisema mambo mengine yaliyofanikisha mtangamano huo ni muundo wa kijamii na kitamaduni wa watu wake, pamoja na mchakato wa kufanya uamuzi kutoka chini kwenda juu unaohusisha kanuni ya maridhiano.

Alikuwa akizungumza na ujumbe kutoka Jamhuri ya Guinea uliofanya ziara ya kikazi katika makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha.

Ujumbe kutoka Jamhuri ya Guinea uliojumuisha makamishna wa uhamiaji, polisi na forodha ulilenga kufanya majadiliano na wawakilishi kutoka Kituo cha Kujenga Uwezo wa Afrika mjini Moshi, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wawakilishi kutoka Kituo cha Kujenga Uwezo wa Afrika mjini Moshi, Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretarieti ya EAC, Kiongozi wa ujumbe kutoka Guinea aliipongeza Sekretarieti ya EAC kwa kazi kubwa iliyofanya iliyoleta hatua kubwa na muhimu katika mchakato wa mtangamano.

“Madhumuni ya ziara yao yalikuwa kupata maelezo ya maendeleo makubwa katika mchakato wa mtangamano pamoja na changamoto zilizojitokeza ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hususani katika masuala ya biashara na forodha, amani na usalama, uhamiaji pamoja na kubadilishana uzoefu sawa na Ecowas,” ilieleza EAC.

Niyonzima alipongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya EAC na jumuiya nyingine za kikanda na kimataifa ikiwamo Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Ukanda wa Afrika Magharibi (Ecowas) ambazo shughuli zake zina mchango katika malengo ya jumuiya hiyo.

Aliwaeleza kuhusu hatua kuu za mtangamano zinazofanyika katika mchakato wa mtangamano hususani utendaji kazi wa Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mipango ya amani na usalama.

“Hii ni pamoja na kushirikiana kupambana na uhalifu wa kimataifa na kuvuka mipaka kama vile biashara ya dawa za kulevya na binadamu, uhamiaji haramu, utakatishaji fedha, uhalifu wa mtandao na wizi wa magari,” alieleza.

Niyonzima aliueleza ujumbe huo juu ya mipango ya ushirikiano kati ya EAC na jumuiya nyingine za kiuchumi za kikanda akisisitiza uanzishwaji wa Eneo Huria la Biashara Tatu la EAC-COMESA-SADC.

Soko la Pamoja la COMESA-EAC-SADC linajumuisha nchi 26 zenye watu takribani milioni 600 na Pato la Taifa la takribani Dola za Marekani trilioni moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live