Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EAC: Nguzo yetu imeanguka

E3634b7041006597b3bb50c25771f810.png EAC: Nguzo yetu imeanguka

Tue, 28 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimemwelezea Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa kama nguzo kuu ya jumuiya hiyo iliyokuwa imebaki baada ya waasisi wake kutangulia mbele za haki.

Waasisi wa EAC ya zamani ni Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta na Rais wa Kwanza wa Uganda, Hayati Dk Milton Obote.

Katika salamu zao za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli na Watanzania wote kwa ujumla, viongozi mbalimbali wa nchi za EAC walimwelezea Hayati Mkapa kama kioo ambacho nchi hizo zitakitumia katika kuijenga jumuiya iliyo imara kama yalivyo maono na fikra zake kuhusu EAC.

Sudan Kusini Katika salamu zake kwa Rais Magufuli, Serikali ya Sudan Kusini chini ya Rais Salva Kiir ilielezea mshtuko walioupata wananchi wa taifa lake kutokana na mchango mkubwa wa Mkapa kupitia Chama cha Mapinduzi katika kujenga umoja wa chama tawala cha nchi hiyo, SPLM na wananchi wa Sudan Kusini kwa ujumla.

Taarifa iliyotolewa na serikali hiyo ilisema Hayati Benjamin Mkapa alikuwa nguzo kuu ya EAC iliyobaki baada ya waasisi wake kufariki.

“Sudan Kusini tulipata msaada mkubwa kutoka kwa Mkapa kuanzia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kusuluhisha migogoro ndani ya chama tawala cha SPLM, ambapo alitusaidia kuwa kitu kimoja na tulimtegemea kutokana na uhodari wake kusuluhisha migogoro ya kimataifa,” ilisema sehemu ya taarifa ya serikali ya Sudan Kusini jana.

Kenya Kwa upande wa Kenya, Rais Uhuru Kenyatta katika salamu zake za rambirambi alimtaja Mkapa kama nguli wa amani na mshikamano ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika nzima. Kenyatta alisema Mkapa alikuwa kiongozi wa kimataifa ambaye weledi wake katika kazi utabaki kama hazina katika mataifa yote Afrika Mashariki na bara zima la Afrika kwa ujumla.

“Alikuwa nguzo muhimu katika mtangamano wa nchi za EAC akiziwezesha kuwa na umoja, mshikamano, amani na maendeleo kwa ujumla,” ilisema sehemu ya ujumbe wa Rais Kenyatta. Rais wa zamani wa Kenya, Mzee Mwai Kibaki katika ujumbe wake wa kuomboleza kifo cha Mkapa, alimtaja Hayati Mkapa kuwa ‘Mwana wa Afrika’ aliyejitolea kwa ajili ya maslahi ya Waafrika wote bila kujali utaifa wa mtu.

“Hayati Mkapa alikuwa bingwa wa kuleta amani kuanzia nchini kwake, Afrika Mashariki na Afrika nzima,” ilisema sehemu ya taarifa iliyosainiwa na Rais Mstaafu Kibaki.

Mzee Kibaki alimwelezea Mkapa katika kipindi cha kustaafu kwake kuwa alijitolea maisha yake kusuluhisha katika mataifa mbalimbali Afrika, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zimbabwe, Sudan Kusini na Burundi.

Burundi Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye alielezea kifo cha Mkapa kama pigo kubwa kwa mshikamano wa Burundi, uchumi wa Burundi na siasa ya Burundi kwa kuwa alikuwa nguzo ya mshikamano wa Warundi na Afrika Mashariki kwa ujumla.

“Wananchi wa Burundi watamkumbuka Mkapa kutokana na kujitolea kwake kuyatetea maisha yao na alilisaidia taifa la Burundi kukubaliwa kujiunga na jumuiya ya EAC,” aliandika Rais Ndaishimiye katika ukurasa wake wa Twitter.

Uganda Kwa upande wake, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema Hayati Mkapa alishirikiana naye na Rais wa Kenya wakati huo, Hayati Daniel Arap Moi kuihuisha EAC mwaka 1999.

“Alipokuwa Rais wa Tanzania, alishirikiana na sisi kuijenga Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni pigo kubwa katika jumuiya yetu na Afrika,” aliandika Rais Museveni katika ukurasa wake wa Twitter. Rwanda Rais wa Rwanda, Paul Kagame katika ujumbe wake wa kuomboleza kifo cha Hayati Mkapa alisema maumivu ya kuondoka kwa kiongozi huyo hayahisiwi na Watanzania peke yao bali ni wananchi wote wa Afrika Mashariki na Afrika.

“Kuondoka kwa kaka yetu Mkapa ni maumivu kwetu sote, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, alikuwa mwanamajumui mkubwa ambaye mchango wake umevuka mipaka ya Tanzania tangu akiwa madarakani na hata alipokuwa amestaafu,” ilisema sehemu ya ujumbe wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Chanzo: habarileo.co.tz