Makao ya mfalme wa Morocco Jumatano yamesema kwamba taifa hilo litatumia takriban dola bilioni 11.7 za kimarekani ndani ya miaka 5 ijayo, kufanya ukarabati kutokana na uharibifu ulioyosababishwa na tetemeko la ardhi la hivi karibuni.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, mpango huo unalenga watu milioni 4.2 kutoka kwenye maeneo yalioathiriwa zaidi ya Al Haouz, Chichaoua, Taroudant, Marrakech, Qourzazate na Azizlal, kulinagana na taarifa kutoka makao ya mfalme, kufuatia mkutano kati ya Mfalme Mohammed VI, na maafisa wa serikali na wa jeshi.
Mpango huo inahusisha miundombinu mipya inayoendana na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwenye maeneo yalioathiriwa na tetemeko la ardhi, taarifa hiyo imeongeza. Taarifa zimeongeza kusema kwamba mpango huo utafadhiliwa na serikali, msaada wa kimataifa, pamoja na mfuko maalum uliobuniwa baada ya mkasa huo.
Tayari dola milioni 700 zimepokelewa kwenye mfuko huo. Wiki iliyopita makao ya mfalme yalisema kwamba nyumba 50,000 ziliharibiwa na kwamba serikali itatoa makazi pamoja na dola 3,000 kwa familia zilizoathiriwa. Pia ahadi ya msaada wa dirham 140,000 kwa kila nyumba iliyoporomoka, na 80,000 kwa kila iliyoharibika imetolewa.
Tetemeko la ardhi la 6.8 kwenye vipimo vya rikta liligonga Morocco Septemba 8 na kuua zaidi ya watu 2,900, wengi wao wakiwa ni kutoka maeneo yasiyoweza kufikiwa kwa urahisi, kwenye milima ya Atlas.