Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dangote kushawishi uwekezaji Tanzania

42ffec684a3878fd4bfc9f51a5e01dff Dangote kushawishi uwekezaji Tanzania

Tue, 25 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MFANYABIASHARA maarufu Nigeria na bilionea namba moja Afrika, Alhaji Aliko Dangote amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Dangote alitoa pongezi hizo jana baada ya kukutana na kuzungumza na Rais Samia Ikulu, Dar es Salaam jana.

Dangote amewekeza katika kiwanda cha uzalishaji saruji mkoani Mtwara na alimuahidi Rais Samia kuwa kampuni yake ambayo imewekeza nchini Dola za Marekani milioni 770

(sawa na Sh trilioni 1.761), itaendelea kuwekeza katika maeneo mengine ukiwemo mpango wake wa kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea.

“Tutaendelea kuwekeza Tanzania ili kuzalisha ajira, mapato ya nchi na kuinua ustawi wa wananchi wa Tanzania, nadhani anahitaji kuungwa mkono katika hili na tumemuahidi kuwa tutaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa hapa Tanzania ili kuunga mkono anachokifanya, sisi tutazalisha ajira,” alisema Alhaji Dangote.

Alisema kutokana na kubadilika na kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini Tanzania, atawahimiza wafanyabiashara na wawekezaji wawekeze Tanzania kwa kuwa serikali ipo tayari kushirikiana nao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, Rais Samia alimpongeza Alhaji Dangote kwa kuwekeza nchini na alimhakikishia kuwa serikali itahakikisha uwekezaji wake na wawekezaji wengine unalindwa kwa manufaa ya pande zote mbili.

Rais Samia alimuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji),

Geoffrey Mwambe, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Yussuf Masauni, wazifanyie kazi changamoto zote zinazokikabili kiwanda cha Dangote ili kiendelee kuzalisha na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.

Viongozi hao walihudhuria mazungumzo hayo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz