Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dangote katika changamoto ya kiuwekezaji nchini mwake

Aliko Dangote Aliko Dangote

Thu, 1 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Takribani wiki mbili zilizopita, kwenye mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), tajiri mkubwa barani Afrika, Aliko Dangote, alikaribia kulia akizungumzia hali ngumu ya kibiashara anayopitia.

Miezi michache iliyopita, Dangote alitangaza uzinduzi wa moja ya viwanda vikubwa vya kusafisha mafuta barani Afrika kwa lengo la kuzalisha mafuta kwa gharama nafuu kwa wananchi.

Kwa bahati mbaya, tangu uzinduzi wa kiwanda chake cha kusafisha mafuta, Aliko amekumbana na vikwazo vingi vya kibiashara. Serikali ya Nigeria, ambayo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani, ilidai kwamba haina mafuta ghafi ya kumpatia Dangote.

Dangote alikasirika sana aliposikia habari hizi na akaamua kwenda Brazil na Marekani kununua mafuta ghafi. Kwa bahati mbaya, na kwa mshangao wake mkubwa, alipotaka kuingiza mafuta haya ghafi kutoka nchi hizo kwa ajili ya kuyasafisha kwenye kiwanda chake, serikali ya Nigeria ilipinga ikisema kwamba hana leseni za uagizaji. Licha ya hatua zote zilizochukuliwa, kiwanda cha Dangote hakikufanikiwa kupata leseni.

Mfanyabiashara huyo, akiwa anakaribia kutokwa machozi, alisema hakujua kwamba mafia wa mafuta wana nguvu kiasi hicho. Alisema wangeweza kumwambia asianze kujenga kiwanda chake, lakini walimsubiri aanze, ajenge kiwanda, ahusishe wawekezaji kisha mwishowe wamwambie kwamba haiwezekani.

Ingawa huenda asiwe kwenye ukingo wa kufilisika kwa sababu ana biashara zingine, hilo lilikuwa pigo kubwa kwa biashara yake.

Rais Tinubu ajitokeza

Katikati ya vuta ni kuvute na manung’uniko ya Dangote, Rais Bola Tinubu wa Nigeria ameiagiza Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Nigeria (NNPC) kuuza mafuta ghafi kwa Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Dangote kwa sarafu ya nchi hiyo, Naira.

Mshauri Maalumu wa Rais kuhusu Habari na Mikakati, Bayo Onanuga, alitoa taarifa hiyo kupitia ukurasa wake rasmi wa X Jumatatu iliyopita.

Onanuga alisema kuwa hatua hiyo, ambayo ni kuhakikisha utulivu wa bei ya mafuta yaliyosafishwa na kiwango cha kubadilisha dola kwa Naira, ilipitishwa na Baraza la Mawaziri la Shirikisho nchini humo.

Ripoti zinasema kuwa kwa sasa Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Dangote kinahitaji shehena 15 za mafuta ghafi, kwa gharama ya dola bilioni 13.5 kwa mwaka, lakini NNPC imejitolea kusambaza nne tu.

Hata hivyo, Baraza la Mawaziri la Shirikisho limeidhinisha kwamba mapipa 450,000 yanayokusudiwa kwa matumizi ya ndani yauzwe kwa Naira kwa viwanda vya kusafisha mafuta vya Nigeria, kwa kutumia kiwanda cha Dangote kama mradi wa majaribio.

Mvutano unajengeka kati ya Dangote na Rais wa nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu katika bara la Afrika.

Kwa kuumizwa na tuhuma kutoka kwa serikali ya nchi yake kwamba anatafuta ukiritimba kwa kiwanda chake cha kusafisha mafuta alichowekeza dola bilioni 20, Dangote amesema ameacha mipango ya kujenga kiwanda kikubwa cha chuma nchini humo kwa hofu ya tuhuma kama hizo.

Hali ya uchumi ambao umekuwa ukipata shida kuvutia uwekezaji, na hatima ya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote, ambacho ni kikubwa zaidi barani, iko hatarini. Bila hiyo, Nigeria mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ghafi barani Afrika itahitaji kuagiza karibu mafuta yote ya magari.

Msimamizi wa sekta ya mafuta nchini Nigeria amesema Dangote anataka kupigwa marufuku uagizaji wa dizeli ili kuongeza ufanisi wa kiwanda hicho na amehoji ubora wa mafuta yake.

Hii imekuja baada ya bilionea huyo kusema kuwa kampuni ya mafuta ya serikali imeshindwa kutekeleza makubaliano ya kumpelekea mapipa 300,000 ya mafuta ghafi kwa siku.

“Kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta kama hiki kinapaswa kuwa fahari kwa kila mtu,” bilionea huyo alisema, akiituhumu mamlaka hiyo kwa kutaka kuendelea kutoa leseni za uagizaji wa mafuta (chanzo cha mapato kinachonufaisha wasomi wa Nigeria kwa miongo kadhaa) badala ya kuruhusu ukuaji na ustawi wa viwanda vya ndani.

Kwa Dangote, ambaye himaya yake ya kibiashara iliruhusiwa kustawi chini ya tawala zilizotangulia kwa makubaliano ya kuwekeza mabilioni ya dola nchini humo, mgogoro huu umekuja kama mshtuko kwake.

“Kupata upendeleo ni muhimu. Katika uzalishaji wa saruji, daima Dangote alikuwa akituhumiwa kufaidika na ukiritimba,” alisema Antony Goldman, mwanzilishi wa Promedia Consulting, kampuni ya ushauri wa hatari za kisiasa. “Wakosoaji wengine wanasema wanaogopa ukiritimba lakini wanashindwa kutaja hali ya sasa inayotegemea uagizaji na waagizaji.”

Vita kuanzia Julai 2023

Julai mwaka jana, Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Dangote kimezituhumu Kampuni za Kimataifa za Mafuta (IOCs) kwa kukwamisha shughuli zake kwa kukataa kukiuzia mafuta ghafi.

Kampuni ya Dangote ilisema kuwa IOCs inapendelea kuuza mafuta ghafi yao kwa nchi za Asia au kuwataka wanunue kutoka kwenye matawi yao ya kigeni badala ya kuwapa kipaumbele kama ilivyoagizwa Tume ya Udhibiti wa Shughuli za Juu za Kitaifa (NUPRC).

Dangote na kundi lake pia wametuhumu wauzaji wa mafuta kwa biashara za magendo kama vile uagizaji wa dizeli iliyochakachuliwa.

Tangu Sheria ya Viwanda vya Petroli (PIA) ya 2021 kuruhusu uagizaji chini ya masharti fulani, wauzaji wa mafuta waliendelea kudharau kiwanda cha Dangote na hivyo kuagiza mafuta nje.

Hata hivyo, Dangote amewashangaza Wanaigeria wengi baada ya kusema hana nyumba nje ya Nigeria, na kwamba ana nyumba mbili—katika mji wake wa Kano, na Lagos—na anaishi katika nyumba ya kukodi kila anapozuru mji mkuu, Abuja.

Januari mwaka huu jarida la ‘Forbes’ lilimtaja kama mtu tajiri zaidi barani Afrika kwa mwaka wa 13 mfululizo licha ya changamoto za kiuchumi nchini.

Kuongezeka kwa utajiri wa Dangote

Utajiri wake uliongezeka kwa dola milioni 400 mwaka uliopita, na kumfanya kuwa na utajiri wa jumla ya dola bilioni 13.9 (Zaidi ya Sh37.5), Forbes ilisema.

Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 66 alijipatia utajiri wake kupitia biashara ya saruji na sukari na mwaka jana alifungua kiwanda cha kusafisha mafuta katika kitovu cha kiuchumi cha Nigeria, Lagos.

Mwekezaji huyo alitoa taarifa hiyo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Dangote Jumapili iliyopita. Maoni yake yamewashangaza wengi katika nchi ambapo tabaka la matajiri lina sifa ya maisha ya kifahari. Wanaigeria wengi wenye utajiri wanamiliki nyumba London, Dubai, na Atlanta.

Maoni yake yamezua mijadala mingi kwenye mitandao ya kijamii, na baadhi wakisema ni uamuzi mzuri wa kibiashara kwani ni gharama nafuu kulipa kodi kuliko kununua nyumba. Kwa Bwana Dangote, sababu ni rahisi tu kwa kuwa anataka kuona Nigeria ikikua.

“Sababu ya kutokuwa na nyumba London au Amerika ni kwa sababu nilitaka kujikita kwenye viwanda nchini Nigeria," alisema na kuongeza, "Nina mapenzi makubwa na ndoto ya Nigeria na mbali na nyumba yangu Lagos, nina nyingine katika jimbo langu la nyumbani, Kano, na nyumba ya kukodi Abuja.

“Kama ningekuwa na nyumba kila mahali, Amerika na kwingineko, nisingeweza kujikita na kujenga kitu kwa ajili ya watu wangu.”

Hamiliki nyumba nje ya Nigeria

Dangote anajulikana kumiliki nyumba ya kifahari katika eneo maarufu la Banana Island huko Lagos, ambapo Wanaigeria wengi wenye hadhi kubwa pia wanamiliki majumba.

Nyumba yake katika jimbo lake la nyumbani la Kano ni ya kawaida na ilitumika kupokea wageni wake wakati wa msiba wa kaka yake, Sani Dangote, mwaka 2021. Mchambuzi wa masuala ya umma Sani Bala alisema Dangote anaweka mfano mzuri sana. “Wanaigeria wanahitaji kuelekezwa upya kuelewa kuwa kumiliki majumba mengi si mafanikio wakati fedha zinahitajika kwingineko.

“Dangote alisema aliuza nyumba yake huko London mwaka 1996 na nina hakika fedha zilizopatikana kutokana na uuzaji huo ziliwekwa tena kwenye biashara yake—hiyo ndiyo njia sahihi ya kufuata.”

Pamoja na yote hayo, Dangote anapambana na vikwazo vya uwekezaji nchini mwake, Nigeria.

Chanzo: Mwanaspoti