Kijana mmoja nchini Uganda katika jiji la Kampala amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mkunga aliyekua akitafuta kazi katika kliniki yake.
Msemaji wa polisi wa Uganda Fred Enanga amewaambia waandishi wa habari kuwa kijana huyo mwenye miaka 18 alikuwa akijifanya daktari ambaye ana nafasi za ajira katika kituo chake cha matibabu.
Enanga amesema mshukiwa huyo alidai kumiliki kituo kisichokuwepo kiitwacho Medical Scrub Uganda na kuwa alitumia ukurasa feki wa Facebook na kujiita daktari Ronnie ili kuwalaghai waathiriwa.
"Aliwahoji waathiriwa kwa ufupi mtandaoni na kisha kupanga mkutano ili kujadili sheria na masharti yatakaoongoza uajiri wao," Enanga alinukuliwa katika gazeti la The Daily Monitor.
Mtuhumiwa anasemekana kuwabaka wanawake hao walipojitokeza kutia saini mikataba ya kazi hizo feki. Mnamo Machi 21, mshukiwa aliripotiwa kumhoji mkunga mwenye umri wa miaka 21 kutoka jiji kuu la Kampala na kisha kumwalika katika kijiji cha Mukono ambapo alimbaka.
"Baada ya uchunguzi wetu tulitumia kikosi cha maafisa wa angani kumsaka mtuhumiwa huyu ambaye tulifanikiwa kumkamata ambapo tumebaini kuwa hakuwa na mahali pamoja pa kufanyia shughuli zake na kuwa alikuwa analala kwenye nyumba za kulala wageni za bei nafuu katika maeneo ya Kayunga na Mukono,” msemaji wa polisi alisema.
Mtuhumiwa inasemekana kutekeleza uhalifu wake katika maeneo ya Kayunga na Mukono ambayo yako kilomita kadhaa kutoka jiji kuu la Kampala.