Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari aliyegundua vinasaba vyenye kinga ya VVU jela China

90367 China+pic Daktari aliyegundua vinasaba vyenye kinga ya VVU jela China

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shenzhen. Mahakama nchini China jana ilimhukumu daktari mmoja ambaye alidai kuhusika katika upandikizaji wa vinasaba kwa watoto, kwenda jela miaka mitatu kwa kufanya kitendo hicho cha kitabibu kinyume cha sheria.

Dk He Jiankui ambaye aliwashtua Wanasayansi mwaka jana kwa kutangaza kuzaliwa kwa mapacha ambao vinasaba vyao vilidaiwa kuwa na kinga ya virusi vya Ukimwi, pia alitozwa Yuan 3 milioni (Dola za Marekani 430,000), shirika la habari la Xinhua limeripoti.

Alihukumiwa na mahakama ya Shenzhen kwa kufanya marekebisho ya vinasaba vya binadamu kwa lengo la uzazi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za China.

Watafiti wenzake wawili pia walihukumiwa. Zhang Renli alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na kutozwa faini ya Yuan 1 milioni wakati Qin Jinzhou akihukumiwa miezi 18, kusimamishwa kwa miaka miwili na kutozwa faini ya Yuan 500,000.

Watatu hao hawakuwa na sifa za kufanya kazi kama madaktari na walijua kwamba wanavunja sheria na kanuni na maadili, hiyo ni kwa mujibu wa hukumu, Xinhua liliarifu.

Walifanya jambo hilo kwa lengo la “kujipatia umaarufu na manufaa binafsi” na hakika walikiuka kanuni za kitabibu, lilieleza.

Xinhua lilibainisha kwamba mtoto wa tatu kuzaliwa kwa vinasaba vilivyobadilishwa alizaliwa kama matokeo ya majaribio yake, hata hivyo haikuweza kuthibitishwa.

Daktari huyo alitangaza Novemba mwaka jana kwamba  watoto wa kwanza duniani wenye vinasaba vilivyohaririwa walizaliwa mwezi huohuo na kwamba aliwawekea vinasaba vitakavyowazuia kupata virusi vya Ukimwi kwa kuondoa kinasaba fulani kwa mbinu inayojulikana kama CRISPR.

Madai hayo yaliwashtua wanasayansi duniani kote yakiibua maswali kuhusu maadili ya kibaolojia na kuiamsha kamati ya utafiti wa kisayansi ya China.

Wakati kukiwa na malalamiko, alianza kuchunguzwa na jeshi la polisi, serikali iliagiza kusimamishwa kwa utafiti wake na alifukuzwa na chuo kkuu alikokuwa nchini humo.

Uhariri wa vinasaba kwa lengo la uzazi  ni kinyume cha sheria katika nchi nyingi duniani. Wizara ya afya ya China ilitoa kanuni mwaka 2003 zinazokataza uhariri wa vinasaba kwa binadamu, ingawa taratibu hizo zinaruhusiwa kwa malengo yasiyo ya uzazi.

Uhariri wake wa vinasaba vya ulilenga kuwaongezea kinga mapacha dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi lakini lengo hilo lilishindikana na kusababisha kitu tofauti, wanasayansi walisema mwezi huu baada ya utafiti wa awali kuchapishwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz