Kamanda wa Vikosi vya Radiamali ya Haraka vya Sudan (RSF) amesema njia bora ya kuhitimisha mapigano nchini humo ni kuviunganisha vikosi hivyo na Jeshi la Sudan.
Mohammad Hamdan Dagalo (Hemedti) alitoa pendekezo hilo jana Jumanne katika ujumbe wa sauti alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kuwa: Tunaipigania Sudan, lakini mabaki (akirejelea Jeshi la Sudan) wanapigana kwa ajili ya mamlaka.
Huku akikanusha madai kuwa vikosi vyake ndivyo vilivyoanzisha vita hivyo, Dagalo amedai kuwa idadi ya wanapiganaji wake wameonegezeka maradufu, na kwamba kuna haja ya wao kujumuishwa kwenye Vikosi vya Jeshi la Sudan (SAF) ili kupunguza taharuki nchini.
Hitilafu kati ya Abdul Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala ambaye pia ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Sudan, na Mohammad Hamdan Daghlo (Hamidati), Kamanda wa vikosi vya RSF zilijitokeza baada ya kusainiwa mkataba wa kuunda kipindi cha mpito na kukabidhiwa madaraka kwa raia. Dagalo (kushoto) na Burhan
Haya yanajiri huku Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) vikizidisha mashambulizi ya anga na ya mizinga kwenye maeneo ya Wanajeshi wa RSF katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.
Maelfu ya watu wameuawa na maelfu ya wengine wamejeruhiwa, huku zaidi ya milioni nne wengine wakiyahama makazi yao ikiwa ni pamoja na Wasudan zaidi ya milioni moja ambao wamekimbilia nchi jirani kutokana na kushadidi vita na mapigano nchini humo.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) linakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 1.8 watakuwa wameikimbia Sudan kutokana na mapigano hayo ya silaha ya kuwania madaraka nchini humo, yaliyoanza Aprili 15.