Verified NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni, Christophe Lutundula, amesema Jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) lililotumwa katika eneo lenye migogoro limeshindwa kutoa matokeo yaliyotarajiwa.
Amesema hayo akiashiria kwamba, huenda EACRF likalazimika kuondoka nchini humo mwishoni mwa mwezi Juni. Hata hivyo, Katibu Mkuu wa EAC, Dk Peter Mathuki, amesema maoni DRC kuhusu jeshi la kanda si ya haki.
Radio ya Ufaransa (RFI) ilimnukuu Mathuki akisema: “Kusema kwamba jeshi la kikanda halifanyi lolote, kwa muda mfupi kama huo, si sawa…”
Awali katika mkutano na waandishi wa habari mwanzoni mwa wiki mjini hapa, Lutundula alisema wanajeshi wa EAC walishindwa kukabiliana na waasi wa M23 kijeshi.
“Ni rahisi, wao (wanajeshi wa EAC) hawajatoa matokeo yaliyotarajiwa,” alisema. “Ninazungumza kwa uwazi. Ni wazi kama maji kwenye glasi safi. Vinginevyo, hatungezungumza tena kuhusu M23. Haihitaji maandamano yoyote maalumu,” alisema.
Kikosi cha kikanda cha EAC kilitumwa Novemba 2022, kikiwa na jukumu la kuunga mkono mchakato wa amani ambao ungefanya M23 kujiondoa.
Kikosi hicho kinachojumuisha wanajeshi kutoka Kenya, Uganda, Burundi na Sudan Kusini kimepata baadhi ya nafasi zilizoachwa wazi na waasi katika kujiondoa kwao taratibu.