Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema rais wa Rwanda Paul Kagame 'ana uwezo wa kusema lolote' kuhusu uchaguzi wa Congo ujao utakaofanyika mwakani.
Patrick Muyaya alikuwa akijibu matamshi ya Jumatano ya Kagame ambaye alisema mwenzake wa Congo hakushinda uchaguzi wa Desemba 2018 na "anajaribu kutafuta njia ya kuahirisha uchaguzi ujao" kwa kuishutumu Rwanda kwa kuhusika na ukosefu wa usalama mashariki mwa Congo.
"Inaweza kuwa bora ikiwa angeangalia [nchi] yake kwanza, ikiwa watu wana uhuru wa kujieleza, kama wako huru kuandamana, na kama anaweza kuvumilia upinzani wowote kwa mawazo yake ya kipekee," Bw Muyaya aliwaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa.
Kinshasa inaishutumu Kigali kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 ambao Muyaya aliwaita "wanajeshi wa Kagame" ambao sasa wanadhibiti eneo lenye utajiri katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Congo, kile ambacho Bw Kagame amekanusha katika matamshi yake.
Bw Muyaya alimshutumu Kagame kwa "kuanzisha ukosefu wa usalama nchini congo" na kujaribu "kumvuruga kisiasa Tshisekedi ... na kuingilia uchaguzi ujao".
Bw Kagame amesema kuwa Rwanda "haina nia ya ukosefu wa usalama nchini Congo" na kwamba alikuwa na nia ya "kitongoji cha amani".
Mvutano kati ya Kinshasa na Congo umeongezeka huku jumuiya ya nchi za Afrika mashariki na rais wa Angola wakijaribu njia ya kidiplomasia kuumaliza.