Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaituhumu nchi ya Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaoendelea kupambana na wanajeshi wake, katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Patrick Muyaya msemaji wa serikali ya Congo amedai kuwa, kundi la waasi wa M23 linapata msaada kutoka nchi jirani ya Rwanda. Kwa upande wake Christophe Lutundula Waziri wa Mashauri ya Kiigeni nchini humo naye ameituhumu serikali ya Rwanda akisema kwamba inawasaidia waasi hao kuvamia kambi ya jeshi ya Rumangabo.
Hata hivyo serikali ya Rwanda imekanusha kuhusika katika mzozo huo kati ya M23 na serikali ya Kinshasa. Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo amesema nchi yake “haina nia ya kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchini Congo.
Mapigano haya yamezua wasiwasi miongoni mwa wakaazi wa maeneo kadhaa katika jimbo la Kivu Kaskazini, ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao huku kukiwa na hofu kuwa huenda waasi hao wakaingia mjini Goma, kama ilivyokuwa mwaka 2012.
Mapigano hayo yameripotiwa kuongezeka zaidi Mei 23, 2022 hasa majira ya usiku huku waasi hao wakidhibithi sehemu za mpakani karibu na Uganda na Rwanda.
Waasi wa M23 wanapigana na wanajeshi wa serikali, ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walipokutana jijini Nairobi, Kenya kuanzisha mazungumzo ya kuleta amani na kutaka kundi la M23 na makundi mengine ya wanamgambo kuweka chini silaha mara moja. Viongozi hao vile vile walikubaliana kuunda kikosi cha jeshi kukabiliana na na waasi hao.