Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DRC yaishutumu Rwanda kwa 'shambulio la ndege zisizo na rubani' katika mji wa Goma

Rais Wa DRC Tshisekedi Anamlinganisha Kagame Wa Rwanda Na Hitler DRC yaishutumu Rwanda kwa 'shambulio la ndege zisizo na rubani' katika mji wa Goma

Sun, 18 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeishutumu Rwanda kwa kufanya shambulizi la ndege isiyo na rubani iliyoharibu ndege ya raia katika uwanja wa ndege katika mji wa kimkakati wa mashariki wa Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini.

Mapigano yalipamba moto katika siku za hivi karibuni karibu na mji wa Sake, kilomita 20 kutoka Goma, kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali ya Kongo. Serikali ya DRC inasema Rwanda inawaunga mkono waasi hao wa M23.

Luteni Kanali Guillaume Ndjike Kaito, msemaji wa jeshi katika jimbo la Kivu Kaskazini amesema kuwa, "Usiku wa Ijumaa hadi Jumamosi, saa 2 asubuhi saa za eneo, kulitokea shambulio la ndege isiyo na rubani; Jeshi la Rwanda limetekeleza shambulizi hilo."

Aliongeza kuwa, "Ni wazi ndege hiyo isiyo na rubani imetoka katika ardhi ya Rwanda, na hivo imekiuka mamlaka ya kujitawala Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,"

Ndege hizo "zililenga ndege za jeshi la DRC", hatahivyo ndege za jeshi "hazikugongwa", alisema, lakini akaongeza kuwa, "ndege ya kiraia iligongwa na kuharibiwa".

Serikali ya Rwanda haikujibu mara moja madai hayo.

DRC na Umoja wa Mataifa zimesema Rwanda inawasaidia waasi katika jitihada za kudhibiti rasilimali nyingi za madini, madai ambayo Kigali imekanusha.

Waasi wameteka maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Waasi nchini DRC Kulingana na waraka wa siri wa Umoja wa Mataifa ulioonekana na AFP mapema wiki hii, jeshi la Rwanda linatumia silaha za hali ya juu, kama vile makombora ya kutoka ardhini hadi angani, kusaidia M23.

Ripoti hiyo ilisema, 'Kombora linaloshukiwa kuwa la Jeshi la Ulinzi la Rwanda kutoka ardhini hadi angani" lilirushwa kuelekea kwenye ndege isiyo na rubani ya Umoja wa Mataifa Jumatano lakini halikuweza kuigonga.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilielezea wasiwasi wake wiki hii kuhusu "kuongezeka kwa ghasia" mashariki mwa DRC, na kulaani mashambulizi ya M23 karibu na Goma.

Makumi ya wanajeshi na raia wameripotiwa kuuawa au kujeruhiwa katika mapigano hayo katika muda wa siku 10 zilizopita.

Wiki iliyopita, waandamanaji katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa, walichoma moto bendera za Marekani na Ubelgiji, wakidai kuwa nchi za Magharibi zinatoa msaada kwa Rwanda, nchi jirani inayotuhumiwa kuunga mkono waasi wa M23 wanaotishia amani Mashariki mwa nchi hiyo.

Huku wakitamka nara kama vile "Ondokeni katika nchi yetu, hatutaki unafiki wenu," baadhi ya wanaandamanaji walirusha mawe kuvunja kamera za usalama kwenye moja ya ofisi za kidiplomasia za Marekani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live