Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imetangaza kuanzishwa uchunguzi baada ya waandamanaji kushambulia balozi za nchi za Magharibi na ofisi za Umoja wa Mataifa katika mji mkuu, Kinshasa.
Maandamano yalizuka mjini Kinshasa katika ofisi za kidiplomasia za nchi za Magharibi na baadhi ya mashirika ya kimataifa siku ya Jumamosi, huku vijana wenye hasira wakichoma moto magari kadhaa ya baadhi ya balozi na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO).
Waandamanaji walikusanyika karibu na balozi za kigeni, zikiwemo ofisi za kidiplomasia za Marekani na Uingereza, Februari 9 na 10.
Waandamanaji hao wanayashutumu mataifa kadhaa ya Magharibi kuwa yanahusika katika mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC.
Serikali ya Kkinshasa ililaani ghasi hizo na kuwataka raia kuwa watulivu katika taarifa yake kufuatia mkutano wa dharura wa usalama ulioitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Peter Kazadi.
Taarifa hiyo ilisema: "Rais wa Jamhuri (Felix Tshisekedi) anasema kwamba ingawa tunaelewa baadhi ya kero za wananchi na kile kinachotokea mashariki mwa nchi, hatua za waandamanaji zinakiuka vifungu kadhaa vya sheria za kimataifa."
Siku ya Jumamosi, Bintou Keita, mkuu wa MONUSCO, alilaani vikali mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, akisisitiza kwamba "magari kadhaa" yalichomwa moto wakati wa maandamano.
Alizitaka mamlaka za mahakama za Kongo kufungua uchunguzi kwa nia ya kuwafungulia mashtaka wahusika.
MONUSCO, ambayo imetumwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu 1999, itaanza kujiondoa taratibu kutoka eneo hilo mwezi Aprili.
Maelfu ya watu katika majimbo mawili ya mashariki yaliyoathiriwa zaidi na migogoro ya Kivu Kaskazini na Ituri wanaishi katika kambi.
Msururu wa maandamano yamezuka nchini DR Congo dhidi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, ambacho watu wanakituhumu kwa kushindwa kuzuia ghasia za makundi mengi yenye silaha.
Madola ya Magharibi yanaaminika kuchochoea vita mashariki mwa DRC ili mashirika ya nchi hizo yaendelee kupora utajiri wa madini eneo hilo.