Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DRC kujiunga EAC mwaka huu

475ad3f797f77349aeb04236bc328a85.jpeg DRC kujiunga EAC mwaka huu

Tue, 25 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itapewa uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka huu na kufanya nchi wanachama kufikia saba.

Katibu Mkuu wa EAC, Dk Peter Mathuki amesema ni matumaini ya jumuiya hiyo ndani ya mwaka huu nchi hiyo itakuwa mwanachama kamili, na kwa sasa imeundwa timu maalumu kwa ajili ya kwenda DRC kufanya tathmini ya kutathmini na kuandaa taarifa ya masharti na vigezo kuwezesha nchi hiyo kuwa mwanachama.

Akizungumza wakati wa kutia saini makubaliano kati ya EAC na Ujerumani iliyotoa dola za Marekani milioni 65 kusaidia sekta ya afya katika nchi za jumuiya hiyo, Dk Mathuki alisema tayari ameziandikia nchi zote wanachama kutoa majina ya wajumbe watakaongia katika timu hiyo itakayokwenda DRC.

Alisema ana imani majina hayo yatatumwa mapema na timu hiyo itakwenda DRC kuangalia kama imetekeleza masharti na vigezo vya kuiwezesha kuwa mwanachama wa EAC, na katikati ya mwaka huu itatakiwa kutoa ripoti yake.

Kuhusu msaada wa dola za Marekani milioni 65 kutoka Ujerumani, Dk Mathuki alisema ni kwa ajili maendeleo ya sekta ya afya, maji na teknolojia kwa nchi zote wanachama.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Ujerumani nchini ambaye pia anaiwakilisha nchi yake katika EAC, Regine Hess alisema msaada huo ni kwa ajili ya watu wote wa EAC.

Alisema msaada huo ni kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko na afya kwa ujumla na kusaidia kituo kilichopo nchini Rwanda kusaidia wanafunzi wa EAC kusoma shahada ya uzamili kuhusu chanjo ili chanjo imfikie kila mtu katika ukanda wa EAC.

Tangu mwaka 1999 Ujerumani imetoa zaidi ya dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya kutekelza miradi mbalimbali ya maendeleo katika EAC.

Chanzo: www.habarileo.co.tz