Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DRC: Wazalendo wakabiliana na M23 pembezoni mwa mji wa Sake

Drc Amnestyyyyy DRC: Wazalendo wakabiliana na M23 pembezoni mwa mji wa Sake

Thu, 28 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mapigano mapya yalizuka jana pembezoni mwa mji wa Sake, jimboni Kivu Kaskazini, kati ya waasi wa M 23, wanaoripotiwa kuungwa mkono na serikali ya Rwanda, na Wazalendo wanaoungwa mkono na serikali ya DRC.

Mbali na maeneo yaliyo na Sake, mapigano hayo yaliripotiwa kutokea pia Masisi na Nyiragongo.

Msemaji wa Jeshi la FARDC jimboni Kivu Kaskazini Luteni Kanali Guillaume Njike, alithibitisha kuzuka kwa mapigano hayo, karibu Kilomita 30 kutoka mji wa Goma.

Milio ya silaha nzito zilizotumiwa kwenye mapambano hayo, ilisika hadi katika kambi za wakimbizi nje ya Goma na kuzua hali ya wasiwasi kuhusu usalama wa raia wa kawaida, kwa mujibu wa mashirika ya kiraia.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa pia na mapigano kati ya waasi wa M 23 na jeshi la FARDC, katika Wilaya za Bihambwe na Masisi na kuzua taharuki miongoni mwa wakaazi.

Serikali jijini Kinshasa, imeendelea kuishtumu Kigali kwa kusababisha utovu wa usalama Mashariki mwa DRC kwa kuwaunga mkono waasi wa M 23, madai ambayo Rwanda imeendelea kukanusha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live