Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DRC: Watu 250,000 wayahama makazi yao ndani ya mwezi mmoja

Wakimbizi Drc Drc.jpeg DRC: Watu 250,000 wayahama makazi yao ndani ya mwezi mmoja

Thu, 14 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Eneo la mashariki mwa DRC limetumbukia katika mzozo mkubwa wa kibinadamu, uliochangiwa na kuongezeka kwa ghasia zilizowalazimu watu 250,000 kuondoka makwao mwezi Februari, kulingana na Ramesh Rajasingham, afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyetembelea Goma, ambayo imekuwa kimbilio la waliolazimika kuyahama makazi yao.

Mbali na mji mkuu wa taifa, Kinshasa, mashariki mwa Kongo kwa muda mrefu imekuwa ikivamiwa na zaidi ya makundi 120 yenye silaha ambayo yanajaribu kumiliki sehemu ya rasilimali za eneo hilo huku yakifanya mauaji. Matokeo yake ni mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, ambapo takriban watu milioni 7 wameyakimbia makazi yao, wengi wao wakiwa hawana msaada. Umoja wa Mataifa umelaani kile ulichokiita janga la kibinadamu "lisilokuwa na kifani"

"Inasikitisha sana (na) nilichoona ni hali mbaya sana," Ramesh Rajasingham, mkurugenzi wa uratibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ihusuyo masuala ya kibinadamu, ameliambia shirika la habari la Associated Press.

Rajasingham alikwenda katika jiji la Goma, ambako watu wengi wanapewa hifadhi ya ukimbizi. "Idadi kubwa kama hii ya watu waliotoroka makazi yao kwa muda mfupi haijawahi kuripotiwa," amesema.

Huku kukiwa na mapigano makali na vikosi vya usalama, kundi la waasi la M23 - ambalo ndilo lililotawala zaidi katika eneo hilo na linalodaiwa kuwa na uhusiano na nchi jirani ya Rwanda - linaendelea kushambulia vijiji, na kuwalazimu watu wengi kukimbilia Goma, jiji kubwa zaidi katika eneo hilo lenye wakazi wanaokadiriwa kuwa milioni 2. Mji tayari hauna rasilimali za kutosha.

Wakati M23 imesema inalenga vikosi vya usalama na sio raia, imezingira jamii kadhaa, na karibu nusu ya mkoa wa Kivu Kaskazini uko chini ya udhibiti wake, kulingana na Richard Moncrieff, mkurugenzi wa shirika la kimataifa linalotatua migogoro International Crisis Group (ICG) katika kanda ya Maeiwa Makuu, na kubaini kwamba watu wengi wamekwama na wamenyimwa.

"Tulikimbia ukosefu wa usalama, lakini hapa pia tunaishi kwa hofu ya mara kwa mara," amesema Chance Wabiwa, 20, huko Goma ambako amekimbilia. "Kupata mahali pa amani kumekuwa jambo la kawaida kwetu. Labda hatutapata tena," aongeza kijana huyo.

Alipochaguliwa tena kwa muhula wa pili wa miaka mitano mwezi Desemba, Rais wa Kongo FĂ©lix Tshisekedi aliishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kutoa msaada wa kijeshi kwa waasi. Rwanda inakanusha madai hayo, lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuna ushahidi mkubwa wa kuwepo kwa vikosi vyao nchini DRC.

Walinda amani wa kikanda na Umoja wa Mataifa walitakiwa kuondoka nchini DRC baada ya serikali kuwashutumu kwa kushindwa kutatua mzozo huo.

Kulingana na Rajasingham, mashirika ya kibinadamu yanafanya kila liwezalo kuwafikia watu walioathiriwa na mzozo huo. Lakini anaonya kwamba "mmiminiko mkubwa wa watu huleta changamoto zaidi ya kile tunaweza kushughulikia kwa sasa."

"Lazima kuwe na suluhu la mateso, kuhama, kupoteza maisha na kupotea kwa elimu," amehitimisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live