Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DRC: Wanajeshi wa Burundi chini ya EAC wameondoka

Vikosi UN Na Drc.jpeg DRC: Wanajeshi wa Burundi chini ya EAC wameondoka

Mon, 11 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Karibia wanajeshi elfu moja wa Burundi chini ya walinda amani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wameondoka nchini DRC, hatua inayokuja baada ya Kinshasa kukataa kuongeza muda wa vikosi vya EAC mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jeshi la Burundi limethibitisha.

Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo ikiwa na wanachama saba, ilituma wanajeshi wake kwa mara ya kwanza mashariki mwa DRC mwezi Novemba mwaka wa 2022 kufuatia wito wa Kinshasa, wakiwa na jukumu la kukomboa vijiji vilivyokuwa vinakaliwa na makundi ya waasi wakiwemo M23.

Wanajeshi hao wamekuwa wakituhumiwa na mkuu wa nchi rais Felix Tshisekedi na raia kwenye taifa hilo kwa kushirikiana na makundi ya waasi na kushindwa kurejesha usalama.

Hatua ya wanajeshi wa Burundi kuondoka imekuja baada ya wenzao wa Sudan kusini karibia 250 na wengine 300 wa Kenya kuondoka baada ya muda wao kumalizika siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita.

Msemaji wa jeshi la Burundi, Kanali Floribert Biyereke, amethibitisha kuwasili salama kwa wanajeshi hao wa Burundi katika nchi yao.

Kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu katika jeshi la Burundi ambaye hakutaka jina lake kutajwa, ameeleza kuwa wanajeshi hao walianza kuondoka nchini DRC siku ya Ijumaa wakitumia malori ya kijeshi yaliopitia katika nchi jirani ya Rwanda kabla ya kuwasili nchini Burundi.

Wanajeshi wa Uganda ambao pia ni sehemu ya EAC, nao pia wanatarajiwa kuondoka nchini DRC katika kipindi cha wiki zijazo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live