Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DRC: Polisi watawanya waandamanaji kwa mabomu ya machozi

Maandamano Upinzani Drc Polisi DRC: Polisi watawanya waandamanaji kwa mabomu ya machozi

Wed, 27 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Polisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo leo Jumatano wamerusha mabomu ya kutoa machozi kutawanya maandamano ya wafuasi wa upinzani katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa, wanaotaka kurudiwa uchaguzi wa rais na wabunge uliokumbwa na machafuko na mvutano mkubwa.

Mzozo huo wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Congo unatishia kuyumbisha zaidi amani na usalama wa nchi hiyo, ambayo tayari inasumbuliwa na matatizo ya usalama katika eneo la mashariki, suala ambalo limetatiza maendeleo na ustawi katika nchi hiyo mzalishaji mkuu wa cobalt na madini mengine duniani.

Wapinzani watano wa Rais Felix Tshisekedi katika kinyang'anyiro hicho pamoja na mashirika ya kiraia, walitoa wito kwa wafuasi wao kujiunga na maandamano hayo leo Jumatano kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu ambayo wanasema yaliandamana na udanganyifu na kwamba yanapaswa kufutiliwa mbali.

Awali serikali ya Congo DR ilikuwa imepiga marufuku maandamano ya kupinga mchakato wa uchaguzi.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ta Congo, Peter Kazadi, alitangaza jana Jumanne kwamba maandamano hayo hayataruhusiwa na kwamba "yanalenga kudhoofisha mchakato wa uchaguzi, na kwamba serikali haiwezi kukubali suala hilo."

Katika barua yao iliyotangazwa kwa umma siku ya Jumamosi iliyopita, wagombea urais watano wa upinzani walimfahamisha Gavana wa Kinshasa kuhusu nia yao ya kuandaa maandamano siku ya Jumatano ili kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu.

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais yanaonyesha kuwa kiongozi wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Bwana Félix Tshisekedi, anaongoza kwa kupata 79% ya kura.

Moïse Katumbi, gavana wa zamani wa eneo lenye utajiri wa madini la Katanga, anatazamiwa kushika nafasi ya pili, kwa asilimia 14 ya kura, akifuatiwa na Martin Fayulu, (4%).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live