Picha za watu waliokuwa wakitoroka katikati mwa Sake kuelekea Goma zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii Jumatano
Mapigano makali katika milima juu ya Bonde la Sake - kitovu kiko kati ya kilomita 20 na 25 magharibi mwa Goma - yamewalazimisha maelfu ya watu kutoroka makwao siku ya Jumatano.
Milio ya risasi nzito na nyepesi iliyosikika kwenye vilima vya Nturo 1, Nturo 2, na maeneo mengine karibu na Sake vimesababisha watu kuogopa na kukimbia, kulingana na mkuu wa kikundi cha kiraia cha Kamuronza - ambapo kitovu cha Sake kinapatikana katika eneo la Masisi - aliyaambia magazeti ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Emile Bolingo, anayeishi katika eneo la Mugunga katika mji wa Goma, ameiambia BBC kwamba watu wengi kutoka Sake walianza kuwasili Mugunga kuanzia saa tatu asubuhi.
Mkuu wa M23, Bertrand Bisimwa amesema kuwa vikosi vyao viliteka kambi za jeshi la serikali kwenye vilima vya "Nturo 1, Nturo 2, na Chez Madimba, juu ya Sake". BBC haikuweza kuthibitisha taarifa hizi kwa vyanzo vinavyojitegemea.
Siku ya Jumanne jioni, msemaji wa jeshi la Congo- FARDC alitangaza kwamba wamerejesha tena kituo kilichopo kwenye eneo la Kirotshe kwenye barabara ya Sake-Minova na wanapigania "kuufungua mji wa Goma na kuachilia barabara zinazoelekea kwenye maeneo ya mazao."