Mamia ya wapiganaji wa kundi la kujilinda kutoka jamii moja ya Congo walijitambulisa kwa mamlaka ya kijeshi ya Ituri siku ya Jumatatu na kutia saini "mkataba wa amani" wa upande mmoja katika eneo hili la kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, linalokumbwa na machafuko.
Wakiwa wamevalia kiraia, bila silaha, watu hawa walifika wakiwa katika magari kadhaa huko Bunia, mji mkuu wa mkoa, huku raia wakishangilia, baadhi yao wakipigwa na mshangao. Magari yalipoingia mjini, maduka na biashara pamoja na soko kuu zilifungwa, amebainisha mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP. Vijana wengi, miongoni mwa wapiganaji hawa walijitambulisha kama wapiganaji kutoka kundi la kujilinda "lililoundwa mnamo mwaka 2019" ili kutetea masilahi ya wanajamii wa "jamii tano waathiriwa wa ukatili huko Ituri".
Kundi hili linalojulikana kama "Zaire", linasema linawakilisha jamii za Hema, Mambisa, Alur, Akongo-Nyali na Ndo-Okebu. "Zaire" ni mpinzani wa kundi lingine lenye silaha la Codeco ("Ushirika kwa Maendeleo ya Kongo"), ambalo linadai kulinda kabila la Lendu dhidi ya Hema na washirika.
Baada ya muongo mmoja wa utulivu, mzozo mbaya huko Ituri kati ya Hema na Lendu ulianza tena tangu mwisho wa mwaka 2017, na kusababisha vifo vya maelfu ya raia na zaidi ya watu milioni moja na nusu kuatoroka makaazi yao. Mzozo wa awali kati ya wanamgambo wa jamii ulisababisha vifo vya maelfu ya watu kati ya mwaka 1999 na 2003, hadi kuingiliwa kati kwa kikosi cha Ulaya, Operesheni Artemis, chini ya usimamizi wa Ufaransa.
"Hapa sisi leo tumejitolea na tuko tayari (kujiunga) na mchakato wa amani" na kushiriki katika mpango wa ujumuishaji wa jamii ambao utaongozwa na mamlaka ya Kongo, ametangaza Jean-Marie Ngadjole, msemaji wa kundi hilo, ambalo linadai kuwa limejitolea "kutowasumbua raia, kuheshimu usafiri huru wa watu na bidhaa zao, jumuiya zote kwa pamoja, katika maeneo ambako tunakoishiā€¯.
Kundi hilo linaomba mamlaka "kuwezesha kuachiliwa kwa wanachama wake wote" waliofungwa na "kuondolewa kwa waranti mbalimbali zilizotolewa" dhidi ya viongozi wake na ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi wa Bunia, amesema Jean-Marie Ngadjole. Jenerali Chalwe Muntutu Ngwashi, makamu wa gavana wa Ituri, amesema "anazingatia" ahadi hii na kuwataka wapiganaji wa kundi hili "kusameheana" na kuboresha "maridhiano".
Baada ya kusaini itifaki, wapiganaji wote waliondoka. Tarehe ya kuwapokonya silaha rasmi haijatangazwa. Mikataba kama hiyo tayari ilitiwa saini na makundi mengine yenye silaha ikiwa ni pamoja na Codeco, bila athari yoyote ya kweli katika uwanja wa vita ambapo ghasia zinaendelea.