Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanajeshi wa serikali FARDC wanasema sasa wanadhibiti mji wa Mushaki uliopo umbali wa Kilomita 40 kutoka Goma, ambao ulikuwa unadhibitiwa na waasi wa M23.
Hatua hii ilikuja baada ya jeshi la Burundi linalounda kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki, kusaidia kuwaondoa waasi hao karibu wiki moja iliyopita.
Jenerali Peter Cirimwami Nkuba, Gavana wa muda wa Kijeshi wa Kivu kaskazini ambaye alitembelea eneo la Masisi mwishoni mwa juma lililopita, aliwakumbusha wakazi wa Mushaki kwamba serikali haitafanya mazungumzo na magaidi wa M23.
‘‘Ni takribani siku nne, tano hivi tangu tufike hapa, tuna amri ya kulisukuma jeshi na jeshi liko hapa. Rais wetu wa Jamhuri na waziri wa ulinzi alisema tuhakikishe usalama hapa MASISI, ili wale wote waliokimbia warudi na kazi iendelee.’’ alisema Jenerali Peter Cirimwami Nkuba.
Nao raia eneo Mushaki, wametoa wito kwa jeshi Congo, kuhakikisha kuwa linadhibiti miji na vijiji vinavyodhibitiwa na M23 mkoani Kivu kaskazini.