Wana umri uliozidi miaka 70 na wakati mwingine hata miaka 100. Watumishi wengi wa umma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hufanya kazi hadi siku zao za mwisho maishani, wakitegemea kinua mgongo na kutambuliwa, vitu ambavyo hawavipati.
"Ningependa serikali imalize ajira yangu kwa heshima," anasema Bayard Kumwimba Dyuba, (84) mwalimu wa shule ya msingi jijini Lubumbashi, mji mkubwa kusini mashariki mwa nchi hiyo kubwa ya Afrika ya kati.
Dyuba ni mtu mfupi mwenye furaha, akiwa na akili ya ujanja, akisumbuliwa na mgongo kupinda na "kusikia kwa matatizo".
"Nilianza kufundisha mwaka 1968, Septemba 9. Ni kazi niliyochagua... sitaki kuiacha," alisema baada ya swali kurudiwa. Anafundisha darasa la wanafunzi 35 wenye umri kati ya miaka 11 na 12. "Lakini niko mwishoni mwa nguvu zangu."
Kwa hiyo, kwanini hastaafu? "Nataka kuondoka," anasema Dyuba. "Lakini si namna hii, bila chochote! Ningepende nipewe nachostahili."
Anakadiria kuwa dola 30,000 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh64 milioni za Kitanzania) zitatosha kuwa mkono wa kwa heri unaostahili kwa ajili ya kuondoka, na baadaye kufuatiwa na pensheni.
Advertisement Lakini kwa miaka kadhaa, walimu wengi na wafanyakazi wa utawala wamesahaliwa, licha ya sheria ya mwaka 2016 kueleza kuwa wale waliofikia umri wa miaka 65 au ambao wamefanya kazi kwa miaka 35 wanaweza kustaafu.
"Tumesahaluliwa, kama tumetupwa," anasema Dyuba, ambaye anasema anapata mshahara wa mwezi wa dola 185 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh370,000 za Kitanzania).
Katika shule nyingine ya msingi iliyo karibu, mwalimu mkuu amefikisha umri wa miaka 78.
Francoise Yumba Mitwele aliingia fani hiyo mwaka 1962. "Ni stadi yangu, napenda kufundisha," anasema, akiwa amevalia nguo ya rangirangi ya mtindo wa Kiafrika.
Kama Dyuba, amechoka lakini anaendelea kufanya kazi akisubiri "donge nono ili aondoke".
Anakadiria fedha hizo ya kumuondoa kufikia dola 25,000 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh50 milioni za Kitanzania), ambazo zitamtosha kunua nyumba kwa ajili ya watoto wake.
Septemba mwaka jana, Waziri wa Utumishi wa Umma, Jean-Pierre Lihau alikadiria idadi ya wafanyakazi ambao wamefikia umri wa kustaafu kuwa watu 350,000.
"Kati yao 14,000 wamevuka miaka 90, wengine 256 wamefikia miaka 100. Mwenye umri mkubwa kuliko wote ana miaka 110," alisema, akifafanua kuwa anataka waanze kuwaondoa taratibu.
"Ilishasikika awali, kila waziri anasema maneno hayohayo na hakuna kinachotokea," alisema mwanasheria anayepinga, Hubert Tshiswaka, mkurugenzi wa taasisi ya uchunguzi wa haki za binadamu jijini Lubumbashi, ambayo inasimamia kesi ya wafanyakazi wa umma waliofikia umri wa kustaafu.
"Pensheni haiji na wababa na wamama wazee wanafariki kwa njia ambayo si nzuri!" Tshiswaka anakosoa wizi wa fedha za umma na wahusika kutochukuliwa hatua.
Mitwele pia haoni matumaini kwa sababu tangu waziri atoe tamko hilo hakuna kilichofanyika.