Chui mmoja amewashambulia watu 13 wakiwemo watoto katika mji wa Alaba Kulito nchini Ethiopia, kilomita 200 kusini mwa mji mkuu Addis Ababa, kabla ya kupigwa risasi na polisi baada ya msako uliodumu kwa saa kadhaa.
Iliripotiwa mara ya kwanza kuwa mnyama huyo alivunja nyumba majira ya asubuhi.
Kisha vikosi vya polisi vilitumwa kudhibiti hali hiyo.
"Alikuwa anaruka juu ya paa la nyumba. Jambo ambalo lilizua taharuki katika jamii. Chui huyo aliyekuwa na hofu akaanza kuwashambulia watu," Naibu Kamanda wa Polisi Taju Negash aliambia BBC.
"Miongoni mwa waathirika walikuwa watoto wawili, na wanawake.
Wengine wakiwa ni vijana," anaongeza. Haijulikani chui huyo alitoka wapi, polisi wanasema.
Waathiriwa kwa sasa wanatibiwa hospitalini.
Matukio kama haya sio kawaida.
Tukio kama hilo mnamo Septemba mwaka jana, chui aliua mume na mke ambao waliokuwa wakirejea nyumbani na kuwajeruhi wanamgambo wengine wawili huko Jimma, magharibi mwa Ethiopia.
Wataalamu wanaonya kuwa mashambulizi ya wanyama yanaongezeka kutokana na baadhi ya watu kujenga nyumba katika maeneo mapya.