Dar es Salaam. Zambia na China zaimarisha uhusiano wao na kuufanya kuwa ule wa “kimakakati zaidi,” huku Rais Xi Jinping akionyesha wazi uungaji wake mkono kwa taifa hilo la Kusini mwa Afrika katika kulinda mamlaka yake, usalama na hivyo kujiletea maendeleo.
Hayo yalisemwa jana Ijumaa Septemba 15, wakati Xi alipokutana na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ambaye yuko ziarani nchini China.
BBC imeripoti kuwa taifa hilo la China, linamiliki hisa nyingi nchini Zambia, na hasa katika sekta ya madini katika kipindi ambacho Zambia inajitahidi kulihudimia deni lake la nje linaloongezeka huku mkopeshaji wake mkubwa akiwa ni China.
Licha ya hayo yote, Rais Xi ameapa kuendelea kufanya kazi na Zambia ili kutanua zaidi wigo wa ushirikiano wa nchi hizo katika nyanja za miundombinu, kilimo, madini, na nishati safi.
Rais Xi amesema urafiki wa China na Zambia "umestahimili dhoruba na changamoto za kimataifa" na kuhimiza uagizaji wa bidhaa zaidi kutoka nchi hiyo ya Afrika.
Kwa upande wake Rais Hichilema amesema Zambia inathamini dhana ya mapinduzi ya kisasa yaliyoibadilisha nchi hiyo, na kwamba anatumai kujifunza kutokana na maendeleo hayo.
Mwaka 2020 wakati wa kipindi cha mlipuko wa ugonjwa Uviko 19; Zambia ilishindwa kulipa deni lake la nje la dola za kimarekani bilioni 18.6; na hiyo kuifanya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika, kushindwa kulipa deni lake, tangu kuanza kwa janga hilo.