Wizara ya Afya nchini Uganda, imesema imepokea chanjo ya kwanza ya Ebola kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, itakayotumika kwa majaribio.
Waziri wa Afya wa Uganda, Jane Ruth Aceng amesema dozi hizo 1,200 zimewasili kutoka kwa Taasisi ya Sabin Vaccine yenye makao yake makuu nchini Marekani.
Amesema “Leo tuna furaha kuwa tuna kundi la kwanza la dawa za chanjo ya Ebola, tutakuwa tukipokea dozi nyingine kutoka kwa Merck na kutoka Oxford.”
Hata hivyo, bado hakuna chanjo zilizoidhinishwa za aina ya Ebola ya Sudan ambayo inasababisha maambukizo hatari nchini Uganda na majaribio hayo yatabainisha kama mojawapo au zote tatu zinafaa katika kupambana na ugonjwa huo.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki imekuwa ikipambana kudhibiti ugonjwa wa Ebola ambao unaambukiza watu tangu mlipuko huo ulipotangazwa mwezi Septemba, 2022.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, kwa sasa hakuna kesi mpya za Ebola na sasa wamefikia siku ya 42 mfululizo bila ya uwepo wa kesi yoyote mpya ya Ebola iliyoripotiwa.