Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, limesema Afrika Magharibi imeorodhesha idadi kubwa zaidi ya vifo vya corona au COVID-19 tangu janga hili lilipoanza huku nchi kadhaa za ukanda huo zinakabiliwa na milipuko mingine ya kipindupindu, ugonjwa wa Ebola na ugonjwa wa Virusi vya homa ya Marburg ambayo inatishia kuongeza shinikizo katika uwezo wa utoaji huduma katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa WHO “vifo vya COVID-19 Afrika Magharibi katika wiki nne zilizopita vimeongezeka kwa asilimia 193% kutoka vifo 348 katika wiki nne zilizopita hadi vifo 1018 katika wiki iliyoishia tarehe 15 Agosti.”
Shirika hilo limeongeza kuwa ingawa uwiano wa vifo, au idadi ya watu waliogunduliwa kuambukizwa ugonjwa ambao wamekufa, inasalia kuwa asilimia 1.4% chini ya wastani wa bara hilo ambao ni asilimia 2.5% hata hivyo limesema hiyo ni asilimia kubwa kuliko mawimbi mawili ya awali katika ukanda huo mdogo na ni ishara kwamba mifumo ya afya mifumo inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka na visa hivyo.
“Ingawa idadi ya wagonjwa wapya huko Afrika Magharibi imeshuka wiki hii, wagonjwa walikuwa wakiongezeka kwa wiki nane mfululizo” limeongeza shirika hilo la kimataifa. Uchomaji wa chanjo ya COVID-19 unaendelea duniani kote, ikiwemo nchini Ivory Coast kama inavyoonekana kwenye picha
Hali halisi ya COVID-19 Kwa ujumla WHO inasema bara la Afrika limerekodi zaidi ya wagonjwa wapya 244,000 katika wiki inayoishia 15 Agosti, ikiwa imeshuka kwa asilimia 11% ikilinganishwa na wiki iliyotangulia na ni wiki ya pili mfululizo yawagonjwa wapya kupungua.
Lakini shirika hilo la afya limeonya kwamba “Katika nchi tisa kati ya 23 zinakabiliwa na wimbi jipya la mlipuko Afrika Magharibi huku Cote d'Ivoire, Guinea na Nigeria zinakabiliwa na ongezeko kubwa la wagonjwa na nchi zote tatu pia zinakabiliana na milipuko mingine ya magonjwa.”
Mifumo ya afya ya Afrika Magharibi ni dhaifu zaidi kuliko ile ya maeneo mengine na tathmini ya (WHO) juu ya utendaji wa mifumo ya afya Afrika Magharibi iligundua kuwa wako chini kwa asilimia 21% ikilinganishwa na Kusini mwa Afrika.
"Tuna wasiwasi sana juu ya Afrika Magharibi na tunaweza kutarajia shinikizo la COVID-19 kuathiri vibaya huduma za afya na kwa kasi zaidi," amesema Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa kanda ya Afrika wa WHO. Ameongeza kuwa "Mbali na shida ya COVID-19, kumezuka Ebola na milipuko mingine. Kupambana na milipuko mingi ni changamoto kubwa na ngumu”
Uwasilishwaji wa chanjo za COVID-19 Shirika la afya limesema “Afrika Magharibi hadi sasa imepokea karibu dozi milioni 29 za chanjo ambayo ni karibu sawa na Afrika Mashariki na Kusini. Hata hivyo WHO imesema usambazaji umekuwa polepole, ambapo ni asilimia 38% tu ya watu wameshapokea chanjo ikilinganishwa na asilimia 76% Mashariki na Kusini mwa Afrika na asilimia 95% Afrika Kaskazini.”
Afrika Magharibi imetoa dozi 2.4 kwa kila watu 100 wakati Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, idadi hiyo iko katika dozi 4.8 kwa kila watu 100.
Usafirishaji wa chanjo barani Afrika umeongezeka kufuatia mchakato wa kituo cha COVAX kikitoa karibu dozi milioni 10 kwa Afrika hadi kufikia mwezi Agosti, hiyo ni mara tisa zaidi ya ile iliyotolewa katika kipindi kama hicho cha Julai mwaka jana.
Muungano wa Afrika AU kwa upande wake hadi sasa umefikisha dozi milioni 1.5 kwa nchi tisa.
Tangu Juni, idadi ya dozi inayotolewa kwa kila watu 100 Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara imeongezeka karibu mara tatu kutoka dozi 1.2 kwa watu 100 hadi 3.4 kwa watu 100.
"Wakati usafirishaji wa chanjo ya COVID-19 unaonekana kuanza, Afrika inakabiliwa na upepo mkali. Hoja za nchi zingine ulimwenguni kuanzisha dozi ya ziada ya kuongeza kinga inatishia ahadi ya kesho njema kwa Afrika. Kwa sababu nchi tajiri ndizo zinazohodhi chanjo, na hufanya kejeli ya usawa wa chanjo, "amesema Dk Moeti.