Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Burundi yaituhumu Rwanda, kufadhili waasi

Rwanda Yamkosoa Rais Wa DRC Kwa Kumfananisha Rais Kagame Na Hitler Burundi yaituhumu Rwanda, kufadhili waasi

Sat, 30 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye ameituhumu nchi ya Rwanda kwa kukifadhili kikundi cha Waasi cha Red-Tabara, kinachofanya mashambulizi ya ardhini na kusababisha vifo vya raia wake.

Hata hivyo, Serikali ya Rwanda amekanusha tuhuma hizo huku ikitoa taarifa isemayo “Rwanda haihusiki kwa njia yoyote na kundi linaloishambulia Burundi.” Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP.

Red - Tabara walifanya mashambulizi Desemba 22, 2023 karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kusababisha vifo vya watu 22 ikiwemo wanawake na watoto.

AFP imeripoti kuwa Ndayishimiye ametoa shutuma hizo katika hotuba yake kwa wananchi kupitia vyombo vya habari na kurushwa moja kwa moja kupitia televisheni na redio ya taifa, akiwa mkoani Cankunzo kwenye mpaka wa Burundi na Tanzania.

“Kikundi hiki cha waasi kimekuwa kikipewa malazi, chakula, ofisi na fedha kutoka nchi inayowasaidia. Namaanisha Rwanda,” amesema Ndayishimiye huku akiongeza kuwa watapigana na waasi hao kwa nguvu zao zote.

Hata hivyo shutuma hizo zimekanushwa si tu na Serikali ya Rwanda, bali pia na waasi wa Red - Tabara wamejitenga nazo.

Kikundi hicho ambacho kimekuwa na makazi yake mashariki mwa DRC katika Mji wa Kivu ya Kusini, kiliibuka mwaka 2011 na hadi sasa ni miongoni mwa makundi yanayofanya mashambulizi zaidi nchini Burundi, huku kikikadiriwa kuwa na wapiganaji kati ya 500 na 800.

“Niliwaambia Rwanda wanapaswa kujua kuwa kuendelea kumsaidia mtu anayeua watoto ni sawa na kupanda mbegu ya chuki kwa watu wa nchi hizi mbili,” amesema Ndayishimiye.

Amesema kwa miaka ya sasa, Burundi imekuwa ikijaribu bila mafanikio kuishawishi Kigali kukikabidhi kikundi hicho cha waasi ili kiweze kukabiliana na mkono wa sheria.

Kwa mujibu wa Serikali ya Burundi, waliouawa Desemba 22, 2023 katika Mji wa Vugizo, walikuwa ni raia na kulikuwa na watoto 12 na wanawake watatu, ambapo wawili kati ya wanawake hao walikuwa wajawazito.

Hata hivyo, kikundi cha Red - Tabara kupitia ukurasa wake katika mtandao wa X, wamechapisha ujumbe uliokana kuhusika na mauaji ya raia yeyote na kusema kuwa kundi hilo halipati msaada kutoka nchi yoyote, linaungwa mkono na Warundi.

Red - Tabara inatuhumiwa kufanya machafuko nchini Burundi tangu mwaka 2015 lakini hakikuwa kikifanya shughuli yoyote nchini humo hadi Septemba 2021, ilipofanya mashambulizi kadhaa, ikiwemo kwenye uwanja wa ndege wa Mji Mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live