BURUNDI inajianda kufanya uchaguzi mkuu wiki hii kuamua nani atachukua nafasi ya Rais Pierre Nkurunziza anayemaliza muda wake,baada ya miaka 15 ya uongozi.
Kampeni zimekuwa na machafuko na vurugu, huku Serikali ikishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu katika jitihada zake za kuendelea kushikilia madaraka.
Kesho wananchi Burundi watamchagua rais mpya. Wakati mataifa mengine yakizingatia kanuni za kukaa mbali, nchini humo, mikutano mikubwa imekuwa ikiendelea bila kuzingatia hilo. Rais wa sasa Pierre Nkurunziza anasema raia wa Burundi watalindwa na Mungu dhidi ya janga la corona.
Katika hali hii ya kutokuwa na wasiwasi, Serikali imetoa taarifa ya kuwa wasimamizi wa uchaguzi kutoka nje lazima wakae karantini kwa wiki mbili pindi wakiingia nchini. Kwa kufanya hivyo kutawazuia kufuatilia uchaguzi huu. Uamuzi huu haujawashangaza wachambuzi wa masuala ya Burundi.
”Tuliyoyashuhudia miezi ya hivi karibuni, ni kwamba mazingira ya siasa Burundi yamefinywa. Tuna wasiwasi ikiwa uchaguzi utakuwa huru na haki, ikiwa watu watamchagua mgombea wanayempenda. Kwa kuwa hakutakuwa na wafuatilaji wa uchaguzi watakaoruhusiwa nchini kushuhudia yanayojiri, nafikiri itaongeza uwezekano wa wizi wa kura, ufisadi na ukiukaji wa haki za kibinadamu katika uchaguzi huu,” ameeleza Nelleke Van De Walle ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Crisis Group.
Kuna wagombea saba wa nafasi ya urais, lakini ni wawili tu wanaobashiriwa kuwa na uwezekano wa kuchaguliwa. Hawa ni Evariste Ndayishimiye, Katibu Mkuu wa Chama cha CNDD-FDD na Agathon Rwasa, kiongozi wa Chama kikuu cha upinzani cha CNL.
Wagombea wote wawili wameeleza uhakika wao wa kutwaa ushindi, lakini hata hivyo kwa Rwasa imekuwa ni kizungumkuti. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema serikali imetumia nguvu zake kutishia na kugandamiza upinzani na wafuasi wake.
Kwa mujibu wa Shirika la Human Rights Watch, kumekuwa na mauaji yasiyopungua 67 yaliyorekodiwa, yakiwemo mauaji 14 yaliyohusishwa na maafisa wa serikali katika miezi 6 iliyopita. Pia kumekuwa na ripoti za watu waliotoweka, matukio ya uteswaji na zaidi ya watu 200 wa upinzani kukamatwa na kuzuiliwa.
Maofisa wa usalama, pia wameshutumiwa kwa kutumia nguvu kupindukia kuzima maandamano au hata mikutano ya upinzani. Dk.Hassan Khannenje ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Horn International.