Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Burundi: Waziri mkuu wa zamani mafichoni, serikali yamsaka

Burundi: Waziri Mkuu Wa Zamani Mafichoni, Serikali Yamsaka Burundi: Waziri mkuu wa zamani mafichoni, serikali yamsaka

Thu, 20 Apr 2023 Chanzo: Voa

Maafisa wa Burundi Jumatano wamesema msako umeanzishwa dhidi ya waziri mkuu wa zamani Alain Guillaume Bunyoni, miezi saba baada ya kufutwa kazi katika harakati za kisiasa za kuwatenga baadhi ya vigogo serikalini.

Bunyoni, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa polisi na waziri wa usalama, alifutwa kazi mwezi Septemba katika mabadiliko ya kwanza makubwa katika serikali ya Burundi tangu Rais Evariste Ndayishimiye achukue hatamu za uongozi mwaka wa 2020.

Polisi na maafisa wa upelelezi walisaka nyumba tatu za Bunyoni siku ya Jumatatu, lakini hawakujua mahali alipotorokea, kwa mujibu wa vyanzo vya usalama na ripoti za vyombo vya habari.

Waziri wa usalama Martin Ninteretse aliwambia waandishi wa habari “Ukweli ni kwamba, ofisi ya mwendesha mashtaka inamshuku jenerali huyo wa polisi kwa makosa fulani na walitaka kumuhoji juu ya makosa hayo. Walifanya msako nyumbani kwake, lakini sikupewa ripoti.”

Amesema ofisi ya mwendesha mashtaka “haijamuelezea kwa nini wanamsaka kwa sababu hawakumpata,” akiongeza kuwa wanasubiri matokeo ya msako huo.

Waziri huyo mkuu wa zamani alionywa mapema kwamba kuna msako mkubwa dhidi yake, na alitoroka kabla ya polisi kufika nyumbani kwake, afisa wa ngazi ya juu katika jeshi ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la AFP.

Afisa huyo amesema maafisa walimkamata afisa wa ngazi ya juu wa polisi akidaiwa kumtaarifu Bunyoni kuhusu operesheni ya kumtafuta.

Waziri Ninteretse aliwambia waandishi wa habari kwamba afisa wa polisi wa cheo cha kanali aliwekwa kizuizini, lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu sababu za kukamatwa kwake.

Bunyoni, kigogo mwenye ushawishi mkubwa katika chama tawala cha CNDD-FDD ambaye aliteuliwa kama waziri mkuu mwaka wa 2020, alifutwa kazi siku chache baada ya rais Ndayishimiye kuonya kuhusu “jaribio” la mapinduzi dhidi yake.

Bunyoni alionekana kama kiongozi wa watu wenye msimamo mkali miongoni mwa majenerali wenye mamlaka ya kweli ya kisiasa nchini Burundi, huku Ndayishimiya mwenyewe akiashiria kutengwa kwake katika hotuba ya mwaka wa 2021.

Ndayishimiye alichukua madaraka mwezi Juni mwaka wa 2020 baada ya mtangulizi wake Pierre Nkurunziza kufariki kutokana na kile maafisa walisema ni mshutuko wa moyo licha ya uvumi uliosambaa kwamba alifariki kutokana na Covid 19.

Huku waziri mkuu wa sasa Gervais Ndirakobuca akiondolewa vikwazo alivyochukuliwa na Marekani na Umoja wa Ulaya tangu mwaka wa 2016, Bunyoni bado iko chini ya vikwazo vya Marekani, kwa tuhuma za kuhusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa maandamano ya mwaka wa 2015 ya kupinga muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza.

Chanzo: Voa