Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza kwamba kundi la mataifa yanayochipuka kiuchumi (Brics) litapokea wanachama wapya sita, ikiwa ni pamoja na Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE) na Iran, mwanzoni mwa mwaka 2024.
Takribani nchi 40 duniani zimeonyesha nia ya kuwa wanachama huku 23 zikiwa tayari zimetuma maombi yao. Wanachama wa Brics wamekubaliana kulipanua kundi hilo kwa kuongeza wanachama wapya.
Katika mkutano huo uliofanyika leo Alhamisi Agosti 24, 2023 huko Johannesburg, Afrika Kusini, viongozi zaidi ya 50 kutoka mataifa yasiyo wanachama wa Brics wamehudhuria akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Tumeamua kuzikaribisha Argentina, Misri, Ethiopia, Iran, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa wanachama kamili wa Brics. Uanachama wao utaanza rasmi Januari Mosi, 2024,” Rais Ramaphosa aliuambia mkutano wa kilele mjini Johannesburg.
Wito wa kupanua Brics inaundwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, ulikuwa umetawala ajenda katika mkutano huo wa siku tatu na kufichua mgawanyiko kuhusu kasi na vigezo vya kupokea wanachama wapya.
Lakini kundi hilo ambalo hufanya uamuzi kwa makubaliano, lilikuwa limekubaliana juu ya “kanuni elekezi, viwango, vigezo na taratibu za mchakato wa kuipanua Brics,” amesema Ramaphosa.
Takriban nchi 23 zilikuwa zimetuma maombi rasmi ya kujiunga na kundi hilo ambalo linawakilisha robo ya uchumi wa dunia na zaidi ya watu bilioni tatu.