Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bomu lililotegwa garini laua watu 9 waliokuwa wakitazama fainali ya Euro

Bomu Lililotegwa Garini Laua Watu 9 Waliokuwa Wakitazama Fainali Ya Euro.png Bomu lililotegwa garini laua watu 9 waliokuwa wakitazama fainali ya Euro

Mon, 15 Jul 2024 Chanzo: Bbc

Watu kadhaa wameuawa baada ya bomu lililotegwa ndani ya gari kulipuka nje ya mkahawa maarufu uliokuwa umejaa mashabiki wa soka katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Bomu hilo lililipuka Jumapili usiku saa 22:28 kwa saa za huko wakati walinzi wa Top Coffee walikuwa wakitazama fainali ya kandanda ya Euro 2024 kati ya Uhispania na England.

Polisi wamesema takriban watu watano waliuawa katika mlipuko huo na wengine 20 kujeruhiwa. Vyanzo vya usalama baadaye vililiambia shirika la habari la AFP kwamba idadi ya waliofariki imeongezeka hadi tisa.

Kundi la wanajihadi la al-Shabab lilisema lilitekeleza shambulio hilo.

"Tulisikia mlipuko mkubwa na wa kutisha katika kipindi cha kwanza cha mchezo tuliokuwa tukiutazama. Kila mtu alilazimika kufikiria jinsi ya kujiokoa," mmoja wa walionusurika, Mohamed Muse, aliiambia BBC.

"Niliona watu katika hatari, watu waliojeruhiwa wakipiga kelele kuomba msaada, na wengine kuchanganyikiwa – ilikuwa hali ya kutisha," aliongeza.

Mlipuko huo pia uliharibu magari kadhaa na kuharibu majengo pia.

Al-Shabab, kundi ambalo ni sehemu ya al-Qaeda, linaripotiwa kusema lililenga mahali ambapo maafisa wa usalama na wafanyikazi wa serikali hukutana usiku.

Eneo hilo liko karibu na Villa Somalia, makazi rasmi ya rais.

Kundi hilo la kijihadi limefanya mashambulizi mengi ya mabomu katika mji huo na maeneo mengine ya Somalia katika kipindi cha miaka 17 iliyopita.

Hata hivyo, kumekuwa na utulivu katika miezi ya hivi karibuni huku kukiwa na kuendelea kwa mashambulizi ya vikosi vya usalama vya Somalia dhidi ya kundi hilo ambalo bado linadhibiti maeneo makubwa ya nchi.

Chanzo: Bbc