Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bomba la mafuta Tanzania, Uganda sasa kumekucha

F66efab2065c70e67d9f7c7216130ca6 Bomba la mafuta Tanzania, Uganda sasa kumekucha

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UAMUZI wa mwisho kuhusu uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) katika mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) utafanyika mwezi ujao.

Hatua hiyo ni ya mwisho kabla ya kuanza rasmi ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445 ambalo litasafirisha mafuta ghafi kutoka Kabaale nchini Uganda hadi Rasi ya Chongoleani iliyo karibu na Bandari ya Tanga, Tanzania.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Mataragio wakati akitangaza fursa kwa wenye viwanda nchini wanaotaka kutengeneza vifaa kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa bomba la gesi litakalojengwa sambamba na bomba hilo la mafuta.

Alisema katika mradi huo wameshakamilisha taratibu zote na kinachosubiriwa kwa sasa ni uamuzi wa mwisho kuhusu uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ambao utafanyika mwezi ujao.

Alisema mradi huo wa EACOP ukikamilika kutajengwa bomba la gesi sambamba na bomba hilo kwa lengo la kusafirisha gesi asilia kutoka Tanzania kwenda Uganda na kusambazwa nchini humo.

“Lengo la kusambaza gesi asilia kwenda nchi mbalimbali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha kusambaza gesi asilia,” alisema. Alisema serikali ina lengo la kupeleka gesi asilia katika nchi jirani ambapo kwa Kenya litajengwa bomba maalumu, pia kwa taifa la Msumbiji na kwa Uganda litajengwa bomba sambamba na la EACOP.

Novemba, mwaka jana, Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini Uganda, Mary Kitutu alitangaza kuwa FDI katika mradi huo itafanyika katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa sekta ya mafuta na gesi wa Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokana na janga la corona, Kitutu alisema mwaka uliopita ulikuwa na changamoto nyingi katika mradi huo kutokana na janga la corona ambalo limeathiri vibaya sekta ya mafuta na gesi.

“Kwa kuwa shughuli zimeanza kwenda vizuri nina matumaini kwamba kufikia robo ya kwanza ya 2021, FDI itakuwa imefanywa, tunafanya kazi kwa bidii kuifanikisha.

Bomba hilo la kihistoria Afrika Mashariki ni la uwekezaji wa zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.5.” “Mradi huu utatoa fursa nyingi za kibiashara ndani ya nchi na ukanda mzima wa Afrika Mashariki na ndio mkataba mkubwa zaidi wa kibiashara kati ya Uganda na Tanzania,” alisema.

Akizungumzia fursa zilizopo kwenye mradi huo, Kitutu alisema serikali ya Uganda inatoa nafasi kwa kampuni za ndani kushiriki katika mradi huo na inafanya kazi kwa karibu na Chama cha Wachimbaji Madini Uganda na vyama vingine vya sekta hiyo ili kuhakikisha kampuni za nchi hiyo zinashiriki.

“Serikali imetenga nyongeza ya ziada ya dola za Marekani bilioni 20 kiasi ambacho kitatumika kusaidia kampuni za za hapa nchini katika maeneo ya miradi ya mafuta na gesi,” alisema.

Kitutu alisema serikali za Uganda na Tanzania zilisaini makubaliano ya mradi wa EACOP Mei, 2017 na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo Agosti, mwaka huo huo.

Mradi huo hata hivyo haukuweza kuendelea kutokana na masuala ya kisheria na mazingira. Septemba, mwaka huu Uganda na Tanzania zilisaini Mkataba wa Serikali Wenyeji (HGA) ili kuharakisha maendeleo ya mradi huo.

Ujenzi wa mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati ya kampuni ya Total (asilimia 66.7) na CNOOC (asilimia 33.3). Bomba hilo la kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi kwa siku

Chanzo: habarileo.co.tz