Mwanamume mmoja aliuawa siku ya Mwaka Mpya baada ya kushambuliwa na simba karibu na Mbuga ya Wanyama ya Shimba Hills huko Matuga, Kaunti ya Kwale.
Mwili wa mwanamume anayeaminika kuwa mwendeshaji bodaboda ulipatikana Jumatatu asubuhi, mita chache tu baada ya pikipiki kupatikana imewachwa barabarani eneo la mbuga hiyo.
“Tulipokea ripoti kutoka kwa wanachi kuwa kuna pikipiki nyekundu iliyolazwa kwa barabara ya Kwale kuelekea Kinango katika eneo la Msitu wa Marere,” ripoti ya polisi ilisema.
Polisi baadaye waligundua nyayo za miguu ya simba na kuzifuata hadi walipopata mwili wa mwanamume aliyekuwa amejeruhiwa na simba huyo.
Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Kwale Stephen Ng’etich alisema mamlaka inayoongozwa na Shirika la Huduma ya Wanyamapori (KWS) imethibitisha kuwa kuna simba mmoja anayezurura katika Kaunti ya Kwale.
Bw Ng’etich aliwataka wakazi kuwa waangalifu na kuepuka barabara hasa nyakati za usiku.
“Tumethibitisha kuwa kuna simba anayezurura mtaani na tunaposubiri timu kutoka Nairobi kumfuatilia, tunaomba wakazi wazuie kutumia barabara hiyo. Akipatikana atahamishiwa kwingine,” Bw Ng’etich alisema na kuongeza kuwa walinzi wa KWS sasa wanachunga maneno hayo.
Mwili wa mwanamume huyo, aliyejeruhiwa kichwani, miguuni na tumboni sasa umelazwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kwale ukisubiri uchunguzi wa maiti na kutambuliwa na familia yake.
Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda Kwale Nehemiah Kinywa aliwataka waendesha bodaboda kuwa makini wanapotumia barabara hiyo.
“Tunawaomba wanachama wetu wote kuwa waangalifu na kuepuka kutumia barabara hasa nyakati za usiku kwa usalama wao,” alisema Bw Kinywa.
Wakazi pia wameombwa kuwa macho simba huyo anapoendelea kutafutwa.
Mwaka jana, wakazi walilalamikia ndovu kuvamia nyumba zao, huku wakulima wakihatarisha maisha yao kulala nje wakilinda mazao yao yasiharibiwe na wanyama hao.