Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodaboda aliyerudisha milioni 115 alizookota, Maisha yanazidi kumpa nafasi

Emmnuel Tuloe Emmanuel Tuloe

Mon, 4 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hadithi ya kile kilichotokea kwa Mliberia Emmanuel Tuloe ina ubora wa hekaya ya kisasa.

Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 19, aliyevalia sare ya shule ya shati la bluu na kaptula, anaonekana tofauti kiumri na wenzake anaosoma nao katika darasa moja.

Lakini kijana huyo aliyewahi kuacha shule ya msingi wakati fulani anaonekana mwenye furaha.

Mwaka jana, alikuwa akihangaika kutafuta riziki akiwa dereva wa pikipiki ndipo alipookota kiasi cha dola za Kimarekani 50,000 (£40,000) katika mchanganyiko wa noti za Marekani na Liberia, zikiwa zimefungwa kwenye mfuko wa plastiki kando ya barabara.

Angeweza kuweka mfukoni kwa urahisi kiasi hiki cha kubadilisha maisha yake. Lakini alimpa shangazi yake azitunze na mmiliki halali alipoomba usaidizi wa kutafuta fedha hizo kwenye redio ya taifa, Emmanuel alijitokeza.

Baadhi ya watu walimkejeli kwa uaminifu wake, wapo waliomcheka wakisema atakufa masikini. Lakini kitendo chake kilimletea zawadi kubwa ikiwa ni pamoja na kupata nafasi katika Taasisi ya Ricks, mojawapo ya shule za kifahari zaidi nchini Libeŕia.

Rais George Weah alimkabidhi dola 10,000 na mmiliki wa vyombo vya habari vya ndani pia akampa zawadi ya Fedha, ambazo baadhi yake zilipatikana kutoka kwa watazamaji na wasikilizaji. Alierudishiwa zilizokuwa zimepotea pia alitoa bidhaa zenye thamani ya $1,500.

Zaidi ya hayo na pengine muhimu zaidi, chuo kimoja nchini Marekani kilijibu kwa kumpa ufadhili kamili wa masomo mara tu atakapomaliza elimu yake ya sekondari.

'Kufurahia nidhamu ya kitaaluma'

Na hilo ndilo analozingatia katika shule ya Ricks, shule ya bweni iliyoanzishwa miaka 135 iliyopita kwa ajili ya wasomi wa jamii ya Liberia waliotokana na watumwa walioachiliwa huru walioanzisha nchi hiyo.

Majengo yake ya ghorofa mbili yamekaa kwenye kampasi nzuri, umbali wa kilomita 6 kutoka pwani ya Atlantiki.

"Ninafurahia shule, si kwa sababu Ricks ina jina kubwa bali ni kwa sababu ya taaluma na maadili," Emmanuel alisema

Kama vile watoto wengi wa Kiliberia kutoka katika mazingira duni ya vijijini wanalazimishwa kufanya hivyo, aliacha shule akiwa na umri wa miaka tisa ili kupata pesa za kusaidia familia yake. Hii ilikuwa muda mfupi baada ya baba yake kufariki kwa ajali ya majini na kwenda kuishi na shangazi yake. Alikua dereva wa pikipiki ya abiria miaka michache tu baadaye.

Baada ya muda mrefu nje ya mazingira ya elimu, anahitaji msaada mkubwa wa ziada shuleni.

Emmanuel alipojiunga na darasa la sita kwa mara ya kwanza "alikuwa akijiona duni; hakuweza kujieleza darasani, lakini siku baada ya siku tulimfanyia kazi", mwalimu wake mkuu Tamba Bangbeor alieleza

"Kielimu, alikuja na msingi mdogo, kwa hivyo tulijaribu kumuweka katika mpango wa uboreshaji. Hiyo imekuwa ikimsaidia."

Sasa ana miaka sita ya shule ya upili mbele yake na atakuwa na miaka 25 atakapohitimu. Lakini hajali pengo la umri na wanafunzi wenzake na anawaelezea kama "marafiki".

Emmanuel pia anafurahia bweni, akisema kwamba "maisha ya bweni ni mazuri kwa sababu hii ni njia ya kujifunza kuishi peke yako siku moja".

Akiangalia siku za usoni, anataka kusomea uhasibu chuo kikuu "kujitayarisha kusaidia kuongoza matumizi ya fedha za nchi".

Busara na uaminifu wake ulionekana kuwa mifano ya kuigwa katika nchi ambayo tuhuma za ufisadi zimekithiri na mara nyingi viongozi wanatuhumiwa kuiba rasilimali za serikali.

'Ni vizuri kuwa mkweli'

Akitafakari jinsi baadhi ya watu walivyomdhihaki kwa kurudisha fedha hizo, anakiri kwamba angeweza kutumia fedha hizo kuboresha hali yake "lakini isingeweza kunipatia fursa niliyonayo sasa".

Emmanuel alimshukuru Mungu kwa kumpa malipo hayo na pia alisema "ninawashukuru wazazi wangu kwa kunifundisha kuwa mwaminifu".

"Na ujumbe wangu kwa vijana wote ni: Ni vizuri kuwa mwaminifu; usichukue kisicho chako."

Walimu wa Ricks wanathamini Emmanuel kuwa hapo?

"Siyo tu kwamba tumenufaika hivi majuzi kutokana na uaminifu wake kama shule, yeye ni golikipa chaguo la pili kwa timu ya soka ya shule," Bw Bangbeor alisema kuhusu shabiki mkali wa Chelsea, ambaye anacheza katika timu hiyo pamoja na wanafunzi walio karibu na umri wake.

Wanafunzi wenzake Emmanuel pia wanamkaribisha akiwa hapo.

Bethlene Kelley, 11, alimwita "rafiki mkubwa ambaye tunapenda kushiriki naye na kumjali kwa sababu yeye ni mkimya na haongei sana. [Yeye ni] mwaminifu, mwenye heshima na mkweli".

Caleb Cooper, 12 anamshukuru Emmanuel kwa mwenendo wake darasani na bwenini.

"Haibii marafiki," Caleb alisema huku akicheka.

Emmanuel akipata kitu ambacho si chake anaripoti kwa mwalimu, mwalimu asipokuwepo anaweka kwenye meza yao," alisema.

Na kutokana na maisha aliyoyaacha Emmanuel, madereva wa teksi za pikipiki hawaonekani kuwa na kinyongo juu ya matarajio yake mapya.

Mmoja wao, Lawrence Fleming, 30, alisema kwamba aliacha shule akiwa darasa la tisa akiwa kijana na alikuwa amefuatilia kwa karibu hadithi ya Emmanuel.

"Ni jambo jema kwamba Emmanuel amerejea shuleni, tunamshukuru Mungu kwa ajili yake," alisema.

Akiwa amesimama karibu na pikipiki yake aina ya Boxer iliyotengenezwa China kwenye njia panda ya mji wa Brewerville, magharibi mwa Monrovia, alipitisha neno la ushauri.

"Mwache abaki shuleni kwa mustakabali wake na mustakabali wa watoto wake... sasa ana fursa ambayo baadhi yetu hatuna."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live