Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akiwa ziarani nchini Nigeria alikokutana na kufanya mazungumzo na rais Bola Tinubu, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya ECOWAS kuisaidia kurejesha uongozi wa kikatiba katika nchi ya Niger.
Mbali na masuala ya kisiasa, Blinken na Tinubu pia wamejadiliana kuhusu namna ya kushinda ugaidi katika nchi za Afrika Magahribi na ukanda wa Sahel.
Nigeria imekuwa ikikabiliwa na machafuko yanayotekelezwa na makundi ya watu wenye silaha kaskazini mwa taifa hilo, mji mkuu wa Abuja pia ukiripoti visa vya utekaji nyara unaofanywa na magenge yenye silaha ambayo baadae huitisha kikombozi kuwaachia huru.
Mataifa yanayopatikana katika ukanda wa Sahel yamekuwa yakikabiliwa na ukosefu wa usalama ambapo pia mapinduzi ya kijeshi yameshuhudiwa katika nchi 15 wanachama wa Ecowas.
Licha ya kuwa waziri Blinken hatozuru mataifa yalioshuhudia mapinduzi, amezungumzia masuala ya kidemokrasia na mwenyeji wake Tinubu.
Wakati akiwa jijini Abidjan, mapema Jumanne, Blinken alimpongeza rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara kwa mipango yake kukabiliana na itikadi kali katika maeneo ya kaskazini mpaka na Sahel.
Marekani imekuwa ikijaribu kuimarisha ushawishi wake barani Afrika haswa wakati huu inapokabiliwa na upinzani kutoka kwa nchi za Urusi na China.
Baada ya ziara yake Nigeria, Blinken anaelekea jijini Luanda nchini Angola baadaye leo, atakakotamatisha ziara yake ya nne barani Afrika.