Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

#Biashara: Kosa la Kompyuta Lililosababisha Pepsi Kutakiwa Kulipa Dola Bilioni 55.

PEPSI #Biashara: Kosa la Kompyuta Lililosababisha Pepsi Kutakiwa Kulipa Dola Bilioni 55.

Thu, 2 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miaka 28 Iliyopita, ‘Wafilipino Walitangaza Vita’ dhidi ya kampuni hiyo Kampeni na promosheni ililenga kuongeza mauzo, badala yake maofisa wa Pepsi si tu kwamba walichakazwa sokoni, walianza kuhofia usalama wa maisha yao.

Ikiwa imepita zaidi ya miaka 28 tangu kutokea kwa kisa hicho, dunia bado haijasahau kosa la kompyuta lililosababisha wananchi wa Ufilipino kutangaza ‘vita’ dhidi ya kampuni ya vinywaji baridi ya Pepsi.

Mei 25, 1992, programu ya Channel 2 News jijini Manila, Philippibes ilitangaza sehemu ya tangazo ambalo lilikuwa linaruka tangu mwezi Februari mwaka huo. Kila siku, kituo hicho cha habari kiliwakumbushia watazamani juu ya namba ya ushindi katika promosheni ya soda za Pepsi. Kwa kununua soda ya Pepsi kuliwapa wanywaji fursa ya kupata namba maalumu ya bahati kulingana na matangazo yaliyokuwa yanaruka kwenye vyombo vya habari.

Ingawa zawadi nyingi kwa washindi zilikuwa ni angalau dola tano tu kwa fedha za sasa, kulikuwa na fursa ya kushinda hadI dola 40,000 kama dau la juu zaidi katika promosheni hiyo.

Miaka ya tisini, taifa la Ufilipino lilikuwa na uchumi dhaifu na umasikini mkubwa na zawadi hiyo kubwa ilionekana na wananchi walio wengi kama fursa ya kubadilisha Maisha. Ilipofika wakati wa kutangaza, namba 349 ilitangazwa kama namba iliyobeba ushindi kwenye televisheni za taifa hilo, maelfu ya Wafilipino hawakuamini jinsi walivyokuwa wenye bahati.

Namba hiyo ndiyo iliyobeba ushindi mkubwa kwenye promosheni. Asubuhi inayofuata, viwanda na maofisi ya Pepsi jijini Manila yalijazwa na maelfu ya watu waliofika wakiwa na vizibo vyao vilivyobeba namba ya bahati; 349! huku wakitazamia zawadi waliyoahidiwa.

Haikuwepo! Ni watu wawili tu walipaswa kushinda zawadi hiyo kuu katika mpango wa awali wa Pepsi. Badala yake, Pepsi ilifanya makossa na kuzalisha vizibo 800,000 vyenye namba ya bahati ya ushindi. Wanywaji waliarifiwa kuwa kampuni hiyo ilikosea na wakaambiwa waondoke haraka kwenye maeneo hayo. Mikanda ya Polisi ilizungushiwa maeneo yote ya viwanda na maofisi ya Pepsi. Kilichofuatia ni maandamano, fujo, migomo na kesi mahakamani. Mabomu ya kutengenezwa majumbani yalitupwa kwenye viwanda vya soda. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Pepsi mwenyewe alisema ‘’tulipokea vitisho vya kuuawa kila siku kama vile kifungua kinywa’’

Kampeni na promosheni ililenga kuongeza mauzo, badala yake maofisa wa Pepsi si tu kwamba walichakazwa sokoni, walianza kuhofia usalama wa maisha yao.

Kama mshindani namba mbili kwenye soko la Ufilipino baada ya Cocacola, Pepsi walijikita kwenye juhudi kadhaa za kimasoko kujaribu kuongeza sehemu ya soko lake.

Kampeni yao hiyo ya namba ya bahati ilionekana na ilitarajiwa kuwa yenye mafanikio. Pepsi waliona dili tu mbele ya macho yao; wakati huo, Ufilipino lilikuwa soko la 12 la vinywaji baridi kwa ukubwa duniani, lakini Pepsi waliachwa mbali sana na Cocacola kwa kiwango cha soko walilokuwa nalo.

Ahadi ya kushinda chochote kitu kuanzia kiwango kidogo had idola 40,000 iliongeza mauzo ya soda za Pepsi kwa 40% ndani ya muda mfupi na kuongeza soko la Pepsi hadi kufikia 26%. Kuanzia mwezi Februari hadi Mei, watu 51000 walishinda dola 5 huku 17 wakishinda zawadi kubwa ya shindano.

Ili kuamua namba ambayo ingeshinda, Pepsi walitafuta kampuni ya D.G Consultores, kampuni la masoko lenye ofisi zake huko Mexico. Namba za ushindi zilitokana na kompyuta, na kuhifadhiwa kwenye sehemu salama jijini Manila. Kuanzia hapo, orodha ingetumika kuwekwa kwenye vizibo vya soda katika viwanda vya kujaza soda. Kila usiku, namba ya ushindi ilisisitizwa kwenye televisheni.

Kwa namna fulani, kuna kosa lilifanyika kwenye mfumo. Kosa la kompyuta lilifanya kampuni ya uchapishaji kuchapa vizibo 800,000 vikiwa ba namba 349 ambayo ilikuwa ni namba ya ushindi ingawa kati ya vyote hivyo, ni viwili tu vilipaswa kushinda. Hayo ni maelezo ambayo kwa wateja hayaingii akilini, na wasingependa kuyasikia hata kidogo ingawa vizibo vyote hivyo, isipokuwa viwili havikuwa na kodi maalumu ya kiusalama ambayo ingethibitisha kuwa vizibo viwili tu ndivyo vilikuwa sahihi.

Wanywaji hawakujal kwakuwa wao waliona wamepata namba ya ushindi na hivyo wakaanza kudai zawadi ambayo waliahidiwa, ingawa vilichapishwa vizibo laki nane kimakosa, ni watu 486,170 tu ndiyo waliogundua kuwa wameshinda na kutunza vizibo vyao.

Baada ya kubaini balaa hilo, maofisa wa Pepsi waliitisha mkutano wa haraka kuamua wangetatuaje balaa walilosababisha. Kiuchumi, kuweza kuwapa washindi karibu 500,000 zawadi iliyoahidiwa ya dola 40,000 isingewezekana na ingegharimu kampuni hiyo mabilioni ya dola, ambayo kwa fedha za leo inafikia dola bilioni 55. Badala yake, Pepsi walisema kuwa ni kosa la kompyuta na kutoa dola 20 kwa kila mwenye kizibo cha ushindi­–kutoka dola 40,000 kama ishara ya nia njema! Kile kilichotazamiwa kuwa promosheni yenye thamani ya dola milioni 2 iligeuka kuwa ya dola milioni 10– kwa kosa moja tu la Kompyuta.

Ingawa baadhi walikubali zawadi hiyo, wanywaji wengine hawakukubali. Walisema kuwa Pepsi waliwapa tumaini la kuwaondolea umasikini, ambalo hawakulitimiza. Hawakujali kuhusu kosa la kompyuta. Pepsi ni kampuni kubwa ni lazima iwajibike kwa makosa yake, walinanga.

Pepsi wakasema hapana, na ndipo matatizo halisi yalipoanzia. Kilichofuata;

Magari ya kusambaza soda za Pepsi yalikuwa ya kwanza kushambuliwa. Ripoti zinaonesha kuwa walau malori 37 yalipinduliwa, kuchomwa, kupigwa mawe au kuharibiwa na waandamanaji ambao walifurika katika mitaa ya Ufiliupino wakiwa na mabango na vipaza sauti kuelezea hasira yao dhidi ya madhambi ya Pepsi.

Maofisi ya Pepsi yalifuatia kushambuliwa kwa mabomu ya kutengenezwa nyumbani yaliyoangukia kwenye vioo, uwani na kwenye sehemu za mapokjezi. Bomu moja la kurushwa na mkono lilianguka karibu na mwalimu wa shule, na kumuua yeye pamoja na mwanafunzi mwenye umri wa miaka mitano huku likiwajeruhi wengine sita.

Maofisa wa Juu wa Pepsi waliajiri walinzi binafsi, wakawapa silaha makondakta wa malori ya kusambaza soda na kuwaondoa wataalamu wake kutoka nje ya nchi na kuwarudisha makwao, huku likiwaacha wachache tu wakabiliane na hasira za wananchi, ambayo kadiri siku zilivyosonga mbele, zilianza kuwa zenye uongozi na kuchukua sura ya vuguvugu rasmi.

Baadhi ya harakati zilikwenda mbali zaidi na kuunda muungano, lakini mmoja ulikuwa maarufu zaidi ukiitwa Coalition 349, ambao ulichukua hatua mahsusi dhidi ya Pepsi ili kuaibisha kampuni hiyo. Baada ya kumchagua kiongozi wao, Vicente del Fierro Jr., walichapisha mabango na tisheti za kushambulia Pepsi na kuwataka wananchi wasusie bidhaa za kampuni hiyo.

Mwandamanaji mmoja, Paciencia Salem,akiwa na miaka 64 ambaye mumewe aliyekuwa muandamanaji alifariki akitembea kwenye maandamano alisema kuwa kampuni hiyo kamwe haitosamehewa. ‘’Hata ikitokea nimekufa leo, mzuka wangu utarudi kupigana na Pepsi. Ni kosa lao. Si kosa letu. Na hivi wamesema hawalipi. Hiyo ndiyo sababu ya kupambana kwetu’’, alisema.

Ingawa Pepsi wenyewe walikuwa wenye tahadhari kubwa katika kujibu madai ya waandamanaji hao wenye hasira, na kuita ni ‘’upokaji fedha’’, walilazimika kujibu wito wa serikali ya Ufilipino. Seneta Gloria Macapagal Arroyo aliita kosa hilo kuwa ni la kizembe wakati ambao maelfu ya kesi za madai na jinai yanamiminika kwenye ofisi za mwendesha mashtaka wa serikali. Baadhi ya makampuni ya mtaani yaliona fursa, mengine yakiamua kununua vizibo vya wanywaji kwa dola 15 wakitumai kuwa siku moja Pepsi wangekubali kulipa zawadi kamili ya kwenye vizibo.

Moto uliendelea kuwaha hadi mwaka 1993, ambapo mambo yalichukua uelekeo mpya katika vichwa vya habari vya vyombo vya Ufilipino. Disemba mwaka huo, Afisa wa Polisi aliandika ripoti kuwa mabomu na maandamano hayakutokana na waandamanaji. Ripoti ilisisitiza kuwa kilichotokea kilikuja kutokana na hujuma binafsi ambazo Pepsi walijifanyia wenyewe.

Madai hayo yaliyoripotiwa na Chicago Tribune, yalitolewa na Artemio Sacaguing, Mkuu wa Makosa ya Uhalifu Uliopangwa katika Idara ya Upelelezi ya Taifa hilo. Katika maelezo yake, Sacaguing alisema kwa waendesha mashtaka wa jijini Manila kuwa mmoja kati ya walinzi wa Pepsi alisema kuwa anawafahamu watu watatu waliokodiwa na Pepsi kufanya uharibifu dhidi ya mali zao.

Sacaguing alidai kwa kufanya hivyo, kungewaonesha makundi yaliyokuwa yakipambana na Pepsi kama wafanya fujo na kuyafanya yaonekane ya kigaidi ili kuyashinda kwenye kesi mahakamani.

Hata hivyo, haikupita muda mrefu hadi wakuu wa kazi wa Sacaguing walipotupilia mbali madai hayo na kusema kuwa ripoti hiyo imeshatupiliwa mbali. Mwanasheria wa Pepsi alikanusha vikali madai hayo. Seneta Macapagal Arroyo yeye alitoa madai mengine ya tofauti kuwa ni washindani wa Pepsi waliokuwa wanafanya hivyo ili kudhoofisha kampuni hiyo nchini Ufilipino.

Hata hivyo, haukuisha muda sana, taswira mbaya dhidi ya Pepsi ilianza kupungua na mambo kurudi kwenye mstari. Kesi nyingi za madai zilizofunguliwa (689) na kesi za jinai (5200) zilitupiliwa mbali na mahakama. Baada ya kuona kuwa Pepsi hawakuwa na lengo la kwenda popote zaidi ya kuendelea kujikita kwenye soko lake hilo, waandamanaji waliishiwa nguvu na vuguvugu dhidi ya Pepsi lilianza kupungua taratibu. Kufikia mwaka 1994, umiliki wa soko ulianza kuimarika kutoka 17% kabla ya kashfa hiyo hadi 21%.

Mwaka 2006, Mahakama ya Rufaa ilifunga mjadala wa kesi hiyo na kuondoa kabisa uwezekano wa Pepsi kuwajibika, na kusema kuwa hakukuwa na ulazima wa Pepsi kuwalipa wale waliokuwa na namba ya bahati kutokana na kosa la kompyuta. Ilikuwa ni kesi ya muda mrefu, lakini hukumu ilimuacha kila mmoja akifuta jasho na kupumua kuwa balaa lililoanza miaka 12 iliyopita, sasa limefikia kikomo.

Ingawa hayo yote hayakufanya promosheni za aina hiyo kukoma kabisa, na hata leo bado zinaendelea. Mwaka 1996, Pepsi walitoa tangazo la kutoa zawadi kwa watakaokusanya alama nyingi zaidi kwa manunuzi ya bidhaa zao. Katika matangazo hayo, kuna tangazo moja liliahidi kununulia mnywaji ndege ya kivita ya Harrier kwa yeyote ambaye angewasilisha alama milioni 7.

Jamaa mmoja, John Leonard aliamua kununua kila alama kwa dola 10. Baada ya kutumia zaidi ya dola 700,000 kukusanya alama, alikwenda Pepsi na kudai ndege yake, ambapo aliambiwa kuwa zawadi hiyo ilikuwa utani tu na mahakama ikakubaliana na madai ya Pepsi.

Vyanzo: Chicago Tribune, Medium, Mental Floss

Chanzo: www.tanzaniaweb.live