Benin imewaachia huru wafuasi 30 wa upinzani waliokamatwa wakati wa uchaguzi wa 2021 ambao ulimkabidhi muhula wa pili Rais Patrice Talon, chanzo cha mahakama kimesema Jumatano.
Uamuzi huo umejiri wakati wa ziara ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye alikutana na Talon katika mji mkuu wa kibiashara, Cotonou.
Taifa hilo la Afrika magharibi lilisifiwa kwa muda mrefu kwa demokrasia bora ya vyama vingi, lakini wakosoaji wanasema hakuna tena uhuru chini ya utawala wa Talon, tajiri mkubwa kwenye sekta ya pamba mwenye umri wa miaka 64 aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2016.
Mahakama maalum ya uhalifu wa kiuchumi na ugaidi, inayojulikana kama Criet, iliwaachia huru watu 30 ambao walikamatwa wakati wa uchaguzi, na kuwaweka chini ya uangalizi wa muda wa mahakama, chanzo hicho kimesema.
Miongoni mwa walioachiliwa ni viongozi na wanaharakati vijana wa chama cha upinzani cha Democrats party, chama hicho kimelithibitishia shirika la habari la AFP.