China imetoa wito kwa pande zote nchini Gabon kutoa usalama kwa rais Ali Bongo, wito unaokuja baada ya kundi la wanajeshi kudai kumaliza utawala wa sasa kwenye taifa hilo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin ameeleza kuwa nchi yake pia inafuatilia kwa ukaribu hali inayoendelea nchini Gabon.
Beijing inapendekeza kufanyika kwa mazungumzo ya pande zote nchini humo kwa manufaa ya raia na kurejeshwa kwa hali ya kawaida haraka iwezekanavyo.
Bongo aliongoza taifa hilo la Afrika Magharibi kama rais kwa kipindi cha muda wa miaka 14 na alikuwa ametangazwa tena mshindi wa uchaguzi mkuu wa hivi karibuni.
Kiongozi huyo alichaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 2009 baada ya kifo cha baba yake, Omar Bongo Ondimba, amabye alikuwa ameongoza taifa hilo kwa kipindi cha miaka 41.
Rais Bongo alizuru Beijing mwezi April na kukutana na rais Xi Jinping, ambaye alimtaja kama rafiki wa zamani kwa watu wa China.
Xi pia alimsifia rais Bongo kwa mafanikio makubwa katika maendeleo ya taifa lake.
Beijing imekuwa ikitaka uwepo wake kutambulika barani Afrika, waziri wake wa mambo ya kigeni wakati huo Qin Gang akizuru bara Afrika mwaka jana.