Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limekutana katika Mkutano wa 1094 kwa njia ya mtandao kujadili hali ya usalama nchini Somalia na shughuli za kikosi cha mpito cha umoja wa Afrika nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ameshiriki Mkutano uliokuwa ukijadili Taarifa iliwasilishwa na Mahmoud Ali Youssouf, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Djibouti ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama kwa mwezi Julai 2022.
Baraza hilo liliangazia masuala yafuatayo; Hali ya kisiasa ya nchini Somalia na kukamilika kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu, Hali ya Usalama na Maendeleo ya Shughuli za Pamoja katika Kusaidia Mpango wa Mpito wa Somalia na Usanifu wa Usalama wa Kitaifa.
Masuala mengine ni kuangazia hali ya Maendeleo katika utekelezaji wa Pendekezo la Pamoja na Dhana ya Uendeshaji, Masuala yanayohusiana na kuimarisha Hali ya Kibinadamu nchini Somalia na Ufadhili endelevu wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia.