Baada ya Niger kumfukuza balozi wa Ufaransa, Burkina Faso nayo imechukua uamuzi wa kumtimua mwambata wa kijeshi wa Ufaransa nchini humo.
Jana Ijumaa, Baraza la Kijeshi linalotawala Burkina Faso lilimtaka afisa wa kijeshi wa Ufaransa nchini kuondoka katika ubalozi wa Ufaransa mjini Ouagadougou - mji mkuu wa Burkina Faso - haraka iwezekanavyo.
Agizo lililotolewa na Baraza la Kijeshi la Burkina Faso limeitaja kazi ya mwambata wa kijeshi wa Ufaransa katika nchi hiyo kuwa ni "uharibifu".
Uhusiano kati ya Burkina Faso na Ufaransa umekuwa wa mvutano mkubwa baada ya Baraza la Kijeshi kuingia madarakani huko Ouagadougou.
Kwa upande mwingine, kufuatia vitisho vya baadhi ya nchi za Kiafrika zikiungwa mkono na Ufaransa vya kuishambulia kijeshi nchi ya Niger, Burkina Faso imetangaza uungaji mkono wake kwa Niamey dhidi ya uingiliaji wowote wa kijeshi wa Ufaransa.
Nchi ya Burkina Faso, ambayo inatawaliwa na baraza la kijeshi, hapo awali ilitoa taarifa ya pamoja na Mali ikitangaza uungaji mkono wake kwa Niger na kuweka wazi kwamba, inatambua uingiliaji wowote wa kijeshi nchini Niger kama tangazo la vita dhidi Burkina Faso.