Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Balozi wa China awatuliza wafanyabiashara

98200 Pic+balozi Balozi wa China awatuliza wafanyabiashara

Fri, 6 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Balozi wa China nchini, Wang Ke amewataka wafanyabiashara wa Kariakoo kuwa watulivu katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona na kwamba biashara zao zitarudi katika hali ya kawaida baada ya muda mfupi.

Balozi Ke alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu virusi vya corona (Covid-19) ambavyo vimeikumba China hasa katika mji wa Wuhan uliopo katika jimbo la Hubei na kuenea katika nchi nyingine duniani.

Alikuwa pamoja na daktari wa magonjwa yanayoambukiza wa Hospitali ya Nanjing nchini China, Dk Li Ping. Balozi Ke alieleza hatua zilizochukuliwa na serikali ya China za kusitisha uzalishaji na kudhibiti usafirishaji na kwamba zimeathiri uchumi si tu kwa China bali na mataifa mengine yenye ushirikiano na taifa hilo.

Hata hivyo, alisema athari hizo ni za muda mfupi na kwamba mwishoni mwa Februari, asilimia 30 ya kampuni ndogo na za kati zilianza kuzalisha wakati asilimia 95 ya masoko makubwa yakifunguliwa.

“Wafanyabiashara wa Kariakoo wawe watulivu wakati mchakato wa kufungua biashara ukiendelea kufanyika nchini China. Athari hizi za kiuchumi zilikuwa haziepukiki, lakini ni za muda mfupi tu,” alisema Ke.

Kauli hiyo ya Balozi Ke imekuja wiki moja baada ya wafanyabiashara wa Kariakoo kulalamika kwamba mlipuko wa virusi vya corona umeathiri upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko hilo maarufu Afrika Mashariki.

Pia Soma

Advertisement
Mbali na wafanyabishara wa ndani, soko hilo pia hutumiwa na wafanyabiashara kutoka nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Msumbiji, Malawi, Zambia na Zimbabwe ambao hununua bidhaa kama nguo, vyombo vya ndani na vifaa vya kielektroniki.

Takwimu kutoka ubalozi wa China zinaonyesha kuwa kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2017, biashara kati ya Tanzania na China imekuwa ikikua kwa kasi na sasa imefikia Sh9.1 trilioni na kwamba kwa sasa Tanzania ni mshirika mkubwa wa taifa hilo la barani Asia.

“Kila baada ya wiki mbili nilikuwa naingiza dukani mzigo kutoka China, lakini hali imekuwa tofauti kwa zaidi ya mwezi,” alisema Bertha Mushi, mfanyabiashara wa Kariakoo, alipozungumza na Mwananchi wiki iliyopita.

Balozi Ke alibainisha mambo kadhaa ambayo nchi nyingine zinaweza kujifunza kutoka China katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo, kama uongozi thabiti wa serikali ya nchi, udhibiti makini na nidhamu na kujitolea kwa watu wa China.

Mambo mengine ni mikakati ya kisayansi ya kudhibiti ugonjwa wa corona, kiwango cha ukweli na uwazi katika kutoa taarifa zinazohusu virusi hivyo na kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana navyo.

Alisema wakuu wa zaidi ya nchi 170 na mashirika 40 ya kimataifa wametoa salamu za rambirambi kwa China na baadhi yao wametoa mkono wa pole kwa kusaidia vifaa mbalimbali katika mji wa Wuhan.

“Rais John Magufuli aliniambia ‘kwa kuzingatia kwamba China ni ndugu zetu, tutatoa madaktari kwenda kusaidia kupambana na virusi vya corona China wakati wowote’. Taarifa hiyo tumeipeleka Beijing,” alisema Balozi Ke.

Kuhusu Watanzania wanaosoma mji wa Wuhan, Balozi Ke aliwahakikishia ndugu na familia za wanafunzi hao kwamba wako salama na wanapatiwa msaada wa karibu na vyuo vikuu wanavyosoma.

Alisema hali ya mambo imezidi kuimarika mjini Wuhan na wanafunzi takribani 400 kutoka Tanzania wako salama na wanaendelea kupatiwa vifaa vya kujikinga, wasaidizi wa kazi na kupata habari mbalimbali.

“Ni uamuzi mzuri zaidi kwao kuendelea kubaki Wuhan kuliko kurudi nyumbani. Vyuo vyao kwa kushirikiana na Serikali vinawahudumia vizuri, pia, ubalozi wa Tanzania nchini China umekuwa na mawasiliano ya karibu na wanafunzi hao,” alisema Balozi Ke.

Alisema serikali ya China iko makini katika kuangalia usalama wao na afya zao hasa wakati huu ambao kuna mlipuko wa virusi vya corona. Amewataka kujikita katika masomo yao badala ya kuwa na hofu.

“Nadhani sasa wanatakiwa kujikita kwenye masomo yao (kwa njia ya mtandao). Hali inazidi kuimarika Wuhan na serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba virusi vya corona havisambai

Naye Dk Ping alieleza makundi yaliyo katika hali tete zaidi ni wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60 na wale walio na magonjwa sugu.

Viwango vya juu vya vifo kutokana na virusi vimekuwa vya wazee, ambao wanafanya asilimia 21.9 wakati idadi ya watoto wanaopata virusi hivyo imekuwa ikiripotiwa kwa nadra.

Chanzo: mwananchi.co.tz