Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Balozi aanika fursa 14 za biashara Burundi 

78e72308206456a002c391c61cd0a326.jpeg Balozi aanika fursa 14 za biashara Burundi 

Tue, 27 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa ya bidhaa mbalimbali zinazohitajika nchini Burundi na nyingine kusafirishwa mpaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Nchi hiyo imetaja bidhaa zinazohitajika kwa wingi nchini na Watanzania kutakiwa kuchangamkia fursa hiyokuwa ni mchele, mtama mweupe, mahindi, unga wa mahindi, muhogo uliokaushwa (makopa) na unga wa muhogo (udaga).

Nyingine ni maharage, mafuta ya kupikia, chumvi yenye madini joto, mvinyo na vifaa vya ujenzi kama saruji, vigae, mabati na nondo.

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk Jilly Maleko, alisema wakati akizungumza na HabariLEO jana kuwa, bidhaa nyingine zinazohitajika nchini humo ni magodoro, vilainishi vya mitambo na malighafi za kutengenezea mbolea na saruji.

Alisema bidhaa hizo haziishii Burundi tu, bali pia husafirishwa kwenda Jimbo la Kivu Kusini lililopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) linalopakana na nchi hiyo.

“Kuna fursa kubwa kwa Watanzania kufanya biashara na Burundi kwa sababu mahitaji ni makubwa pamoja na Mashariki mwa DRC,” alisema.

Aidha, Balozi Maleko alisema thamani ya bidhaa za Burundi zilizouzwa Tanzania mwaka 2019 ilifikia Sh milioni 831.4, huku Tanzania ikiuza bidhaa nchini humo zenye thamani ya Sh bilioni 200.18.

Alisema kabla ya janga la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Burundi kilikuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka, huku Tanzania ikiuza zaidi nchini humo.

Alitoa mfano kuwa, kuanzia mwaka 2015 hadi 2019, Tanzania na Burundi zilifanya biashara ya Sh bilioni 619.9, ambayo ni wastani wa Sh bilioni 123.9 kwa mwaka.

“Baada ya kutokea mlipuko wa Covid-19, biashara baina ya Tanzania na Burundi imepungua kwa kiwango kidogo kutokana na kufungwa kwa masoko ya mpakani ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona,” alisema.

Hata hivyo, Balozi Maleko alisema bidhaa zinazopita katika Kituo cha Pamoja cha Mpakani (OSBP) cha Kabanga/Kobero na kwenye mpaka wa Manyovu/Mugina zimeendelea kusafirishwa kwenda kwenye soko la kila nchi kutokana na hatua za serikali za nchi hizi kutekeleza makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kuruhusu usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine kuendelea licha ya kuwapo janga hilo.

Alisema Tanzania na Burundi licha ya kuwa ni nchi jirani, zina uhusiano wa kihistoria na wa kindugu na ushirikiano mzuri ambao umeendelea kushamiri katika nyanya za siasa na diplomasia, ulinzi na usalama, uchumi na kijamii.

Aliema tangu ilipopata uhuru mwaka 1962, Burundi imepitia vipindi mbalimbali vya machafuko ya kisiasa yaliyosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na Tanzania imeshiriki kwa karibu katika usuluhishi uliosaidia kusainiwa kwa makubaliano ya amani (Arusha Agreement) mwaka 2000.

Alisema Tanzania pia ilishiriki katika kurejesha amani nchini Burundi kupitia mazungumzo ya amani yaliyokuwa yanasimamiwa na EAC chini ya mwezeshaji aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa na juhudi hizo zimesababisha kurejea kwa amani na utulivu nchini humo.

“Kwa jumla, sasa hali ya kisiasa na kiusalama nchini Burundi ni tulivu na hali ya uchumi inaanza kutengamaa, hii ni fursa nzuri ya kukuza zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii ya nchi zote mbili,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz