Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba wa Mtanzania aliyejinyonga gerezani ahangaikia mwili

2cf3c1a21144d95a669136fbc27eed0a Baba wa Mtanzania aliyejinyonga gerezani ahangaikia mwili

Wed, 2 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

FAMILIA ya Mtanzania Rashid Mberesero aliyefungwa kwa ugaidi ambaye amefariki dunia kwa kujinyonga katika Gereza la Kamiti nchini Kenya, inafanya juhudi za kuweza kuupata mwili wa kijana wao ili wakaufanyie maziko wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Baba mzazi wa Rashid, Charles Mberesero aliliambia HabariLEO jana kuwa juhudi za kuufuatilia mwili wa kijana wake zilianza baada ya kupata taarifa za kifo chake.

Mberesero alisema alianzia Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania kwa lengo la kujua taratibu na mambo ya kufanya ili wapate mwili, na kuelekezwa apeleke maombi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mzazi huyo wa Rashid alisema alikwenda Wizara ya Mambo ya Nje, lakini mpaka tunakwenda mitamboni alikuwa bado yupo wizarani huko kuonana na maofisa ili asaidiwe.

Aidha, Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake nchini Kenya imeiandikia barua Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya kupatiwa maelezo ya kina kuhusu mazingira ya kutokea kwa kifo hicho.

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Talha Mohammed alisema mpaka kufikia jana wizara ilikuwa haijajibu barua hiyo ingawa waliahidi kuwa watawasiliana na mamlaka zinazohusika kama Jeshi la Magereza ili kupata majibu sahihi.

Mzazi wa marehemu alisema alipata taarifa kupitia vyombo vya habari kuhusu kifo cha mwanawe huko Kenya na kuamua kufuatilia taarifa hizo kujua ukweli wake.

“Kwa kuwa sikuwa na mtu wa kuzungumza naye kutoka Kenya ili aweze kunithibitishia niliamua kuja Dar es Salaam (kutokea Kilimanjaro), Mungu akipenda sisi kama familia tutauchukua mwili wa mtoto wetu na kuuzika nyumbani,” alisema Mberesero.

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Kenya alithibitisha kuwa habari rasmi za kifo cha kijana huyo wanazo lakini kuna maswali yapo ndani ya habari hizo na lazima yapatiwe majibu kutoka katika mamlaka zinazohusika.

“Mpaka sasa taarifa tuliyonayo rasmi ni hiyo kwamba ni kweli kijana huyo amefariki dunia kwa kujinyonga na kwamba tunaendelea kusubiri majibu kutoka Serikali ya Kenya kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kuhusu mazingira ya kifo hicho,” alisema Mohammed.

Alisema katika barua hiyo, Tanzania inataka kujua kilichotokea kwa kijana huyo mpaka akapoteza uhai wake na pia kama kuna taratibu zozote zilizoandaliwa kuhusu maziko ya mwili huo.

“Moja ya maelezo tunayohitaji ni ikiwa magereza watahitaji ndugu wa marehemu kwa ajili ya kuwakabidhi na kama ndugu hawatahitaji mwili huo basi watachukua jukumu la kuuzika mwili huo kwa sababu alikuwa mfungwa aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha,” alisema.

Alisema ingawa ofisi ya balozi mjini Nairobi haijapata taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kama ndugu wanafuatilia mwili wa kijana wao, lakini ikiwa watawasilisha maombi watapewa mwili huo lakini kwa gharama zao.

Alitoa rai kwa ndugu na familia ya kijana huyo kama wanahitaji mwili wa mpendwa wao wawasilishe maombi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo kwa mijibu wa taratibu gharama zote za kuuchukua na kuusafirisha mwili huo kuja Tanzania zitalipwa na ndugu wa marehemu.

Rashid alihukumiwa na wenzake wawili Wakenya, Hassan Edin na Mohamed Abdi waliofungwa kifungo cha miaka 41 kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kuhusika na shambulio la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garisa Aprili 2015.

Wakati wa shambulio hilo magaidi waliwaua kwa kuwapiga risasi wanafunzi zaidi ya 500 ambao 150 kati yao ndio waliothibitika kufa. Vijana hao watatu walitiwa hatiani kwa kula njama na kufanya shambulio la kigaidi kwa kushirikiana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab lenye maskani yake katika nchi jirani ya Somalia.

Chanzo: habarileo.co.tz